Amri ya Kim Jong-un ya kuimarishwa uwezo wa jeshi la Korea Kaskazini

Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini ametoa amri ya kuimarishwa uwezo wa jeshi la nchi hiyo kwa ajili ya kukabiliana na adui.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limetangaza kwamba Kim Jong-un ametoa amri hiyo kufuatia hatua ya Marekani kutwaa meli ya kubeba mizigo ya serikali ya Pyongyang kwa kisingizio kuwa imekiuka vikwazo vilivyowekwa.

Kufuatia hatua hiyo kiongozi huyo amesisitiza udharura wa kuongezwa uwezo wa vikosi vya ulinzi vilivyo katika mstari wa mbele na ngome ya Magharibi kwa lengo la kuwa tayari kutelekeza operesheni za kiulinzi ili kukabiliana na hali yoyote ile hatari. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Korea Kaskazini imeainisha ajenda yenye kipaumbele muhimu kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake wa kiulinzi. 

Kadhalika Kim Jong-un amebainisha kwamba amani na usalama wa kweli utadhaminiwa kupitia vikosi vya askari wenye uwezo ambao wanaweza kutetea haki ya kujitawala nchi hiyo.

Ikumbukwe kuwa, meli iliyokuwa na mzigo wa tani elfu 17 ya Korea Kaskazini iliyosimamishwa mwaka jana nchini Indonesia kwa tuhuma za kubeba makaa ya mawe, ilitwaliwa na Marekani Ijumaa usiku kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imelaaniwa vikali na serikali ya Pyongyang.

Amri mpya ya Kiongozi wa Korea Kaskazini ya kuimarishwa uwezo wa kiulinzi wa jeshi la nchi hiyo ni sehemu nyingine ya misimamo ya serikali ya Pyongyang juu ya kuendelea mienendo ya uhasama ya Marekani, ukiwemo wa kuvunja mazungumzo ya pande mbili yaliyokusudiwa kutatua mzozo wa nyuklia katika Rasi ya Korea. 

Katika wiki za hivi karibuni na baada ya kufeli duru ya pili ya mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na Kim Jong-un huko mjini Hanoi, Vietnam, Korea Kaskazini ilianzisha tena majaribio yake ya makombora.

Katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya pande mbili nchini Singapore, Pyongyang iliahidi kusitisha majaribio yake ya makombora na silaha za nyuklia, hata hivyo White House ikakiuka ahadi zake kuhusu kusimamishwa vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya Asia ambapo ilirefusha kwa kipindi cha mwaka mmoja mwingine vikwazo vyake dhidi ya Korea Kaskazini.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post