WAZIRI MHAGAMA AWAASA WAFANYAKAZI KUTIMIZA WAJIBU WAO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista mhagama amewaasa wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii na uzalendo ili kuendelea kutimiza wajibu wao na kujiletea maendeleo nchini.

Ametoa kauli hiyo jana Aprili 29, 2019 alipokuwa akihutubia wafanyakazi walioshiriki katika semina maaalum ya wafanyakazi iliyowakutanisha wajumbe kutoka vyama mbali mbali vya wafanyakazi ili kujadili chimbuko la sherehe za wafanyakazi (Mei Mosi) na kujadili masuala ya sheria za kazi katika ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya.

Akizungumza na wajumbe wa semina hiyo, waziri Mhagama aliwaasa wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa weledi na tija ili kuendelea kuwa na taifa lenye maendeleo kwa kuzingatia mchango wa wafanyakazi nchini.

“Wafanyakazi endeleeni kufanya kazi kwa umoja, weledi huku mkizingatia kanuni, taratibu na sheria zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yenu pasipo kukiuka masuala ya msingi yanayowahusu,”alisema Waziri Mhagama.

Aliongezea kuwa, katika kuhakikisha Taifa linakuwa na maendeleo endelevu ni vyema wafanyakazi wakaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia mchango mkubwa wa wafanyakazi nchini katika kujiletea maendeleo kwa kuzingatia tija walioyonayo nchini.

“Niwakumbushe kuwa nyie ni wadau muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na Serikali inawategemea katika kuchangia maendeleo ya nchi hivyo mnapaswa kujali maeneo yenu ya kazi na kuendelea kuvitumia vyama vya wafanyakazi katika kueleza masuala yenu na kutumia vyama vyenu kutatua changamoto zinazowakabili,”alisisitiza Waziri Mhagama

Sambamba na hilo Waziri aliwataka wafanyazkai kuendelea kuzingatia uwajibikaji wenye misingi ya haki na usawa ili kuwa na mazingira salama ya kiutendaji pasipo kuvunja sheria za wafanyakazi ili kuwa na matokeo chanya kama inavyotarajiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUICO Taifa Bw. Paulo Sangeze alieleza shukrani zake kwa namna serikali inavyoendelea kuunga mkono uwepo wa Vyama vya wafanyakazi na kuahidi kutoa ushiorikiano kila itakapohitajika.

“Kwa dhati ya moyo wangu na kwa niaba ya TUCTA ninatoa shukrani kwa Serikali kwa namna inavyounga mkono shughuli za vyama vya wafanyakazi na hakika kumekuwa na mabadiliko makbwa tofauti na ilivyokuwa awali,”alisisitiza bw. Sangeze


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post