WAZIRI ANGELLAH KAIRUKI AZUNGUMZA NA MABALOZI WA NCHI 3 KUHUSU MAMBO YA UWEKEZAJI NCHINI


Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angela Kairuki atakutana na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali waliowekeza Tanzania ili kujua changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa haraka na kuimarisha mahusiano ya nchi hizo na Tanzania katika sekta ya Uwekezaji.

Akizungumza katika mazungumzo mafupi aliyoyafanya jana kwa wakati tafaouti Mabalozi kutoka nchi za Ufaransa, Uholonzi, Norway pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani USAID, Waziri Kairuki alisema kuwa mazungumzo hayo ni chachu ya ushirikiano katika sekta ya uwekezaji nchini.

Katika mazungumzo na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier, Waziri Kairuki alisema kuwa nchi ya ufaransa na Tanzania zina ushirikiano wa muda mrefu katika sekta mbalimbali ikiwemo ya uwekezaji pamoja na biashara.

“Tulikuwa na mazungumzo na Balozi wa Ufaransa ambaye tumejadili mambo mbalimbali katika ushirikiano wetu ili kuwaita wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Ufaransa waje nchi kama ilivyokuwa mwaka jana, ambapo kulikuwa na ugeni wa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka huko na walifanya majadiliano na TPSF, kwa hiyo na mwaka huu tumekubaliana watawaalika tena TPSF na TIC ili kuweza kujadili mambo ya uwekezaji”, Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki alisema kuwa katika kukutana na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kutafungua fursa na namna ya kufuatilia changamoto ili uwekezaji mkubwa uweze kufanyika nchini, pia Waziri Kairuki alieleza kuwa wamekubaliana na Balozi wa Ufaransa kuwa na ugeni mkubwa wa wawekezaji kati ya mwezi Mei na Septemba ambao watakuja kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Aidha Waziri Kairuki alimhakikishia Balozi wa Ufaransa nchi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji kutoka Ufaransa ili kuongeza uwekezaji nchini kutoka wawekezaji 40 na kuongezeka ili kuweka namba kubwa ya wawekezaji kutoka Ufaransa.

“Uwekezaji unaongeza pato letu, unaongeza fedha za kigeni, ajira pamoja na masuala mengine katika uchumi, katika hili Ufaransa wamesema wako tayari kuanzisha jukwaa la biashara kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania na Ufaransa ili kuweza kuvutia zaidi wawekezaji”, Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki aliongeza kuwa Serikali iko pamoja na wawekezaji na amewahakikishia kuwa iko tayari kutatua changamoto zao katika masuala ya uwekezaji ili kuweza kuvutia wakezaji na kuwa mabalozi wa uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier amesema kuwa Serikali ya Ufaransa iko pamoja na itashirikaina na Tanzania katika kitimiza adhima ya Rais Magufuli ya kuifikisha Tanzania uchumi wa kati mwaka 2025.

“Tulikuwa na Mazungumzo ya kubadilishana mawazo kuona namna gani ya kuipeleka Tanzania mbele katika sekta ya uwekezaji, Serikali ya Ufaransa inamuunga mkono Rais, Dkt.John Pombe Magufuli kwa nia yake ya kuipeleka Tanzania mbele kimaendeleo na kuwa nchi ya Uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”, Frederic Clavier, Balozi wa Ufaransa Tanzania.

Aidha Balozi Clavier aliongeza kuwa Serikali ya Ufaransa inawekeza Euro milioni 50 kwa mwaka na itaongeza mpaka kufika Euro milioni 100 ambazo zitatrumika katika uwekezaji mbalimbali hapa nchini ikiwemo Sekta ya mafuta, Viwanda vya Dawa na kilimo.

Katika mazungumzo mengine na Mabalozi wa Uholanzi, Jeroen Verheul, Norway, Elisabeth Jacobsen pamoja na Mkurugenzi Mkazi USAID, Andy Karas, Waziri Kairuki amewahakikishia kuwa atakutana na wawekezaji kutoka nchi hizo, kuwasikiliza changamoto zao na kuzitatua ili kuimarisha sekta ya uwekezaji nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527