SERIKALI YAFAFANUA KATAZO LA MATUMIZI YA MIFUKO YA PLASTIKI


Serikali imejipanga kuhakisha kuwa mifuko mbadala wa plastiki inapatikana kwa wingi ili kukidhi mahitaji. 

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hii leo Jijini Dodoma na kusisitiza kuwa katazo la Mifuko ya Plastiki lililotolewa jana na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa linakuwa na nguvu kisheria kwa kuandika kanuni za katazo ya mifuko ya plastiki zitakazotangazwa katika gazeti la Serikali chini ya Sheria ya Mazingira na kutoa adhabu kwa kila mtu atakaekiuka utaratibu uliowekwa.  

“Kabla ya Serikali kutangaza hatua ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ulifanyika utafiti na maandalizi ya mifuko mbadala. Uwezo wa kuzalisha upo na mifuko ya karatasi inayotumika Kenya na Rwanda inatumia malighafi inayozalishwa Mgololo-Iringa,Tanzania.” Makamba alisistiza

Waziri Makamba ameainisha kuwa kuna vifungashio ambavyo havitapigwa marufuku ambavyo ni pamoja na vifungashio vya dawa za hospitalini, vifungashio katika sekta ya kilimo na ujenzi pia vile vya kuhifadhi maziwa na kutolea mfano wa vifungashio vya maziwa ya ASAS na Tanga Fresh, hata hivyo utaratibu maalumu utawekwa kwa wamiliki wa kukusanya vifungashio hivyo mara baada ya matumizi yake. 

Akizungumzia juu ya ushirikishwaji, Waziri Makamba amesema kuwa zoezi hili limekuwa ni shirikishi na hatua iliyotangazwa na Waziri Mkuu sio ya kushtukiza kwa kuwa Ofisi yake iliratibu mikutano katika maeneo kadhaa nchini kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu zuio la mifuko ya plastiki.

Katika kukamilisha utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Waziri Makamba amesema Ofisi yake imeunda kikosi kazi cha kusimamia katazo hilo kikihusisha wajumbe kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Wengine ni Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema kuwa mapema wiki ijayo ataitisha mkutano wa wawekezaji wa mifuko mbadala kote nchini na kujadili kwa kina namna bora ya kuwekeza katika uzalishaji wa mifuko mbadala rafiki wa mazingira.

Serikali imetangaza kuanzia Juni Mosi 2019 kuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527