SERIKALI YAANZISHA MFUMO WA KIELEKTRONIKI AMBAO MWEKEZAJI ANAWEZA KUOMBA KUWEKEZA NCHINI AKIWA POPOTE DUNIANI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ofisi yake imeanzisha mfumo wa kielektroniki ambao mwekezaji anaweza kuomba kuwekeza nchini akiwa popote duniani.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Jasmine Tiisekwa (CCM).

Dk. Tiisekwa alisema kwa kuwa dira ya maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 ni kufikia uchumi wa kati na uchumi wa viwanda ni kigezo kimojawapo.

“Na kwa kuwa Serikali ya awamu ya tano imejielekeza kwenye uchumi wa viwanda na imejitahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji ili waweze kuja kuwekeza, hata hivyo wawekezaji wengi wanakwamishwa na kusumbuliwa sana.

“Je, nini kauli ya Serikali kuhusu suala hili?” aliuliza Dk. Tiisekwa.

Akijibu, Waziri Mkuu alisema ofisi yake imeanzisha mfumo mpya wa kielektroniki ambao mwekezaji anaweza kuomba kuwekeza nchini akiwa popote duniani.

“Ofisi ya Waziri Mkuu tumeanzisha mfumo wa kielektroniki ambao sasa mwekezaji anaweza kuomba kutoka popote alipo.

“Tunatambua wawekezaji wako nje ya nchi, haimlazimishi yeye kuja moja kwa moja Tanzania kuanza kujaza makaratasi, anajaza huko huko Marekani kuomba nafasi ya kupata ardhi, kupata ithibati ya uwekezaji hapa nchini,” alisema Majaliwa.

Alisema Serikali imetengeneza haya yote kurahisisha mfumo wa uwekezaji kwa lengo la kupanua wigo wa uchumi hapa nchini kupitia viwanda.

“Lakini pia kufungua kupitia kilimo, kupitia madini lakini eneo maalumu mwekezaji anataka kuwekeza, sasa Tanzania imefungua fursa na kutengeneza mazingira rahisi ya uwekezaji,” alisema.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa wawekezaji kuja  kuwekeza Tanzania, ambako alidai fursa ipo na ardhi ipo.

“Na fursa hizi sasa tumezikaribisha katika mikoa na wilaya, tunayo ardhi kwa ajili ya kukaribisha wawekezaji ili kuendelea kuongeza mapato ya halmashauri yenyewe, mikoa yenyewe na taifa kwa ujumla,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527