BUNGE LA UINGEREZA LATAHADHARISHA JUU YA UWEZEKANO WA KUTOKEA VITA VYA SILAHA ZA NYUKLIA DUNIANI


Kamati ya Mahusiano ya Kimataifa ya Bunge la Uingereza imetoa taarifa inayoonya juu ya uwezekano wa kutokea vita vya silaha za nyuklia kati ya nchi zenye silaha hizo.

Kamati hiyo imeeleza kwamba kutokana na kushindikana ushirikiano wa kidiplomasia kati ya nchi zenye silaha za nyuklia na kadhalika kuendelea kustawishwa kila siku teknolojia na uwezo mpya katika uwanja huo, kumeongeza hatari ya kutokea vita vya silaha za nyuklia dunia. 

David Howell, Mkuu wa Kamati hiyo ameitaka serikali ya nchi hiyo kuupa umuhimu wasiwasi wa wawakilishi wa bunge hilo. 

Aidha Howell ametaka kuongezwa kiwango cha mazungumzo kati ya nchi zenye kumiliki silaha hizo za maangamizi. 

Ripoti ya kamati hiyo juu ya uwezekano wa kutokea vita vya silaha za nyuklia imetolewa ikiwa ni miezi michache imepita baada ya kutolewa ripoti iliyosema kuwa, Marekani na Russia ambazo ni wamiliki wakubwa wa silaha za nyuklia, zimesimamisha makubaliano muhimu ya silaha baina yao.

Mwezi Februari mwaka huu, serikali ya Marekani kwa kisingizio cha kuwa eti Russia imekiuka mkataba wa makombora kati ya nchi mbili, ilitangaza kwamba imesimamisha Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati maarufu kwa kifupi kama INF kuanzia tarehe pili Februari na kuanza kutekeleza hatua za kujiondoa kwenye mkataba huo ambazo zitadumu kwa kipindi cha miezi sita. Kufuatia hatua hiyo, Rais Vladmir Putin wa Russia alisisitiza kuwa hatua hiyo haitakosa jibu na kwamba serikali ya Moscow nayo imesimamisha mkataba huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527