SERIKALI YA TANZANIA YASHINDA KESI YA MADAI YA DOLA 55,099,171.66 NCHINI MAREKANI


Mnamo tarehe 12 Februari, 2018 familia ya marehemu Vipula Valambhia ilifungua kesi ya Madai Na. 1:18-CV-370 (TSC) dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mahakama ya District Court of Columbia nchini Marekani. Walalamikiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.


Walalamikaji katika Shauri hili ni Bi. Vipula D. Valambhia, Priscilla D. Valambhia, Bhavna D. Valambhia, Punita D. Valambhia na Krishnakant D. Valambhia ambao ni Mjane na Watoto wanne wa Marehemu Vipula Valambhia aliyefariki mwaka 2005 nchini Marekani. Walalamikaji wote ni raia wa Marekani na wakati wakifungua kesi hii, walikuwa wanaishi Houston, Texas Marekani.

Katika kesi hii, walalamikaji waliwakilishwa na Wakili kutoka Meredith B. Parenti wa Parenti Law PLLC, kutoka Taxes, Marekani. Kwenye mdai yao, Walalamikaji waliiomba Mahakama ya Marekani kupitia Sheria ya Marekani iitwayo Uniform Foreign- Country Money Judgments Recognition Act,DC Codes, . §§ 15-361- 15-371 iweze kutambua na kutoa amri ya kukazia malipo ya fedha Kiasi cha Dola za Marekani 55,099,171.66 zilizoamuriwa na Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka, 2003.

Walalamikaji walidai kuwa, kiasi hicho cha fedha kilipaswa kilipwe tokea tarehe 4, Juni 2001, pamoja na riba ya 7% kila mwaka. Hivyo, wakati wa kufungua shauri hilo, yaani tarehe 19 Februari, 2018, deni halisi lilikuwa ni Dola za Marekani 64,500,750.87.

Madai katika shauri hili yalitokana na Mkataba wa ununuzi wa vifaa vya kijeshi kati ya Kampuni ya Transport Equipment Ltd (TEL) ya Marehemu Vipula Valambhia na Serikali ya Tanzania. Mkataba huo uliokuwa unahusu ununuzi wa vifaa vya jeshi uliingiwa miaka ya 1980 na Kampuni ya TEL ilikuwa ikidai kwamba haijakamilishiwa malipo yote ya fedha zitokanazo na Mkataba huo. Hivyo, Kampuni hiyo iliamua kufungua Kesi Na. 210 ya mwaka 1989 iliyotolewa uamuzi na Mahakama za Tanzania.

Serikali ya Tanzania ilishawasilisha utetezi wake kupinga shauri hilo tarehe 13 Julai, 2018. Katika utetezi huo, Serikali ya Tanzania ilipinga madai hayo ya familia ya Valambhia kwa kuwa yalifunguliwa kinyume cha Sheria na taratibu za Sheria ya Marekani inayotambua na kuruhusu kukazia hukumu za kimahakama zitokanazo na Mahakama za nchi nyingine (Recognisation and Enforcement of Foreign Judgments) nchini Marekani. Serikali ya Tanzania ilieleza kuwa, ina kinga ya kisheria kama Nchi kufunguliwa Madai ya kukazia hukumu za kimahakama nchini Marekani (sovereign immunity), kinga hiyo ambayo inatambulika chini ya Sheria ya Marekani iitwayo “Foreign Sovereign Immunities Act, 28 U.SC. §§ 1602”. (“FSIA” or “Act”).

Mnamo tarehe 31 Machi, 2019, Mahakama ya District Court of Columbia, nchini Marekani chaini ya Mhe. Jaji Tanya S. Chutkan ilitoa uamuzi wake na kuona kuamua kuwa, madai yaliyowasilishwa na familia ya Valambhia hayakukuhusisha shughuli za kibiashara zilizofanyika nchini Marekani kama ambavyo Sheria ya Marekani ya “Uniform Foreign-Country Money Judgments Recognition Act,” inavyotaka.

Walalamikaji walikiri kupitia maelezo yaliyowaslishwa Mahakamani hapo kuwa, Shauri hilo linahusisha suala lililofanyika nje ya Marekani baina ya Kampuni ambayo sio ya Kimarekani na Serikali ya Tanzania.

Katika mazingira hayo, Mahakama iliafikiana na hoja za upande wa Serikali ya Tanzania kuwa, madai ya Familia ya Marehemu Valambia hayana msingi kisheria na kuwa Walalamikaji hawakustaili kufunguliwa kesi ya namna hiyo nchini Marekani. Hivyo, Kesi hiyo ilifutwa Mahakamani hapo kwa ushindi upande wa Tanzania.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post