Ripoti ya CAG: MATOKEO YA UKAGUZI WA MASHIRIKA YA UMMA

5.1 Utangulizi

Sura hii inawasilisha matokeo ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma. Maeneo yaliyokaguliwa ni Mwenendo wa Kifedha na Uwezo wa Kuendelea kutoa Huduma; Usimamizi wa Mapato katika Mashirika ya Umma; Ongezeko la Madeni ya Wafanyakazi katika Taasisi za Elimu ya Juu; Ukamilishaji wa Miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa; Hali ya Mali za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya; Ukusanyaji wa Madeni ya Wateja wa Mamlaka za Maji; na Usimamizi wa Mikataba na Manunuzi katika Mashirika ya Umma.


Ndugu Waandishi wa Habari,
Ukaguzi wa Mashirika ya Umma ulibaini masuala mbalimbali ambayo, Serikali inapaswa kuyafanyia kazi ili kuboresha usimamizi wa Rasilimali za Umma kama ifuatavyo. 

5.2 Udhaifu katika Mwenendo wa Kifedha na Uwezo wa Kuendelea kutoa Huduma 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika ukaguzi wangu, nilibaini kuwepo kwa Mashirika ya Umma 14 yenye matatizo makubwa ya kifedha pamoja na kupata hasara hadi kusababisha madeni kuwa zaidi ya mitaji yao kwa zaidi ya asilimia 100. Aidha, kati ya Mashirika hayo, Mashirika 11 yana ukwasi hasi kwa maana yanajiendesha kwa hasara kwa zaidi ya miaka 2 sasa. Kufuatia hali hii, ni dhahiri kuwa Mashirika hayo hayawezi kujiendesha bila kutegemea msaada kutoka Serikali Kuu. Hivyo, ipo hatari ya kushindwa kuendelea kutoa huduma kwa jamii. Jedwali Na. 14 linaainisha Taasisi zenye hali mbaya kifedha.

Jedwali Na. 14: Taasisi Zenye Hali Mbaya Kifedha

5.3 Udhaifu wa Usimamizi wa Mapato katika Mashirika ya Umma 

Ndugu Waandishi wa Habari, 
Katika mapitio ya usimamizi wa mapato katika Mashirika ya Umma mbalimbali, nilibaini dosari zikiwemo;   

5.3.1 Udhaifu katika ufuatiliaji wa marejesho ya kiasi cha shilingi trilioni 1.46 cha mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeshindwa kufahamu walipo wakopaji wa mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya shilingi trilioni 1.46. Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa sana ikizingatiwa kuwa Kifungu cha 4(h) cha Sheria ya Bodi kinaitaka Bodi kutengeneza mtandao na kushirikiana na Taasisi na Mashirika mbalimbali ili kuwatambua wadaiwa na kuwezesha kupata marejesho ya mikopo hiyo.

5.3.2 Changamoto katika ukusanyaji wa tozo za maegesho ya meli

Mamlaka ya Mapato Tanzania inakusanya tozo za maegesho ya meli kwa niaba ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na kila mwisho wa mwezi Mamlaka ya Bandari Tanzania inafanya uwianishaji wa kibenki. 

Hata hivyo, wakati wa ukaguzi wa mapato ya maegesho niligundua utofauti wa shilingi bilioni 42.5 katika kumbukumbu za Mamlaka ya Bandari Tanzania na zile za Mamlaka ya Mapato Tanzania. Hali hii inatokana na ukosefu wa ushirikiano wa kutosha kati ya Mamlaka hizi mbili katika uwianishaji wa taarifa pindi inapotokea tofauti. 

5.2.1 Udhaifu wa utawala bora katika mashirika ya umma
Kwenye taarifa zangu za ukaguzi kwa miaka ya fedha 2015/16 na 2016/17 niliripoti kuwa Mashirika ya Umma 18 na 20, mtawalia, yalikuwa yakijiendesha bila kuwa na Bodi za Wakurugenzi kwa muda mrefu. 

Nilishauri Mamlaka za Uteuzi kuchukua hatua za makusudi kuteua Wakurugenzi ili kuboresha Utawala Bora na Udhibiti wa Ndani wa Taasisi husika. Katika ukaguzi wangu wa mwaka 2017/18 nimebaini kuwa Mashirika 24 hayakuwa na Bodi za Wakurugenzi. Kati ya Mashirika haya, saba (7) yanafanya kazi bila ya kuwa na bodi kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku Mashirika manne (4) yakiwa na zaidi ya miaka miwili.

5.4 Ongezeko la Madeni ya Wafanyakazi katika Taasisi za Elimu ya Juu 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 2017/18, madeni yanayohusiana na malipo ya posho ya majukumu kwa wahadhiri wa Vyuo Vikuu vya Mzumbe na Ardhi yameongezeka. Katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, madeni yameongezeka kutoka shilingi bilioni 1.49 hadi shilingi bilioni 3.41, na kwa Chuo Kikuu cha Ardhi, madeni yameongezeka kutoka shilingi bilioni 1.48 hadi bilioni 2.26. 

Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Mzumbe vilikuwa na madeni ya kiinua mgongo ya shilingi bilioni 5.59 na shilingi milioni 525, mtawalia kwa wafanyakazi ambao wamemaliza mikataba yao. 

Vilevile, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilikuwa na madeni ya shilingi bilioni 6.78 ikiwa ni posho za nyumba na madeni mengineyo ya wafanyakazi tangu Juni 2017. Hali hii inaweza kusababisha kushuka kwa kiwango cha elimu ya juu kutokana na wahadhiri kukosa morali ya kazi. 

5.5 Ucheleweshaji wa Ukamilishaji wa Miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa 

Ndugu Waandishi wa Habari, 
Shirika la Nyumba la Taifa lilianzisha Mradi wa Nyumba wa Golden Premier Residence (711-2) uliopo Kawe, Kitalu Na. 711/2 mnamo tarehe 16 Oktoba, 2013. 

Katika mapitio yangu, nilibaini mradi huo ulisimama tangu mwanzo wa mwaka 2017 kutokana na ukosefu wa fedha. Hadi unasimama, mradi ulikuwa umekamilika kwa asilimia 30 na umetumia jumla ya shilingi bilioni 34.87, ambapo vyanzo vya ndani vilichangia kiasi cha shilingi bilioni 11.64 na mkopo kutoka Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ulikuwa ni shilingi bilioni 23.23. 

Shirika la Nyumba la Taifa lilitakiwa kuanza kulipa marejesho ya Mkopo kuanzia Julai 2018. Hivyo, Shirika linatumia fedha kutoka vyanzo vingine kulipa mkopo huo huku mradi ukiwa haujakamilika. 

Ikiwa Shirika la Nyumba la Taifa halitapata kibali cha kukopa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kutokana na kufikia ukomo wake wa kukopa, litapaswa kuwalipa wakandarasi jumla ya shilingi bilioni 99.99 kwa kuvunja mikataba. 

Pia, litatakiwa kurejesha jumla ya shilingi bilioni 2.6 kwa wateja waliokwishaanza kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa nyumba hizo. 

5.6 Kupungua kwa Mali za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya

Ndugu Waandishi wa Habari,
Japokuwa makusanyo ya mwaka yanaendelea kuwa makubwa zaidi ya malipo ya huduma za bima ya afya, kwa sasa malipo ya huduma za afya yanakua kwa uwiano mkubwa mwaka hadi mwaka zaidi ya uwiano wa kukua kwa mapato. Kutokana na hali hii, makisio ya madai ya huduma za bima ya afya pekee ifikapo mwaka wa fedha utakaoishia Juni 2024 yatakuwa ni asilimia 99.2 ya jumla ya makusanyo yote. Uwiano huu unakisiwa kuongezeka zaidi hadi kufikia asilimia 104.8 katika mwaka unaofuata. 

Hali hii inamaanisha kwamba madai ya huduma za bima ya afya yanaendelea kuongezeka, na itafikia kipindi ambapo makusanyo na mapato kutoka katika uwekezaji hayataweza kukidhi madai na hivyo itaulazimu Mfuko kuchukua hatua za dharura kama kuuza mali zake.

5.7 Udhaifu katika Ukusanyaji wa Shilingi Bilioni 97.58 za Madeni ya Wateja wa Mamlaka za Maji 

Nilibaini kuwepo kwa kiwango kidogo cha kukusanya marejesho ya madeni ndani ya Mamlaka za Maji, kwa kuwa mapato mengi yalikuwa hayajakusanywa na yamezidi muda uliowekwa kwenye Sera ya Mikopo ya Mamlaka husika. 

Katika jumla ya deni hilo la shilingi bilioni 97.58, nilibaini kuwa shilingi bilioni 39.59 (sawa na asilimia 41) ni Madeni ya Serikali, na shilingi bilioni 57.99 (sawa na asilimia 59) ni madeni ya wateja wengine. Ongezeko hili la madeni limesababishwa na ufuatiliaji hafifu wa wadeni na kutokufuata Sera ya Mamlaka za Maji ya kukata huduma za maji kwa wateja wanaokiuka taratibu. 
  
Udhaifu katika Usimamizi wa Mikataba na Manunuzi katika Mashirika ya Umma
Kampuni Hodhi ya Kusimamia Rasilimali za Shirika la Reli (RAHCO) ilifanya malipo ya awali ya kiasi cha Dola za Marekani 500,000 ikiwa ni sawa na shilingi bilioni 1.07 mwaka 2015 kwa mhandisi mshauri kwa kazi ya kutoa huduma ya ushauri ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge). Hata hivyo, huduma hiyo haikutolewa hadi kufikia Februari 2019, ikiwa ni miaka mitatu tangu malipo yalipofanyika. Mkataba ulikuwa wa miezi 12 kuanzia tarehe ya kusaini mkataba ambayo ilikuwa tarehe 20 Mei, 2015. 

Aidha, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kiliingia mkataba na Kampuni ya SUMSANG C & T Corporation tarehe 16 Desemba, 2014 kwa ajili ya kuleta na kufunga mfumo unaojulikana kama “OCS 121 System Viewer”. Mfumo huu ulifungwa tarehe 26 Julai, 2017 kwa mkataba wa Dola za Marekani milioni 1.41. Hadi kufikia wakati wa ukaguzi, mfumo huo ulikuwa haujaanza kutumika kwa kuwa ulikuwa haujakidhi vigezo vilivyokuwa vimeainishwa kwenye mkataba.  

5.8 Mapendekezo 
Ndugu Waandishi wa Habari,

Ili kurekebisha kasoro zilizobainishwa katika ripoti hii, ninaishauri Serikali ihakikishe: 
(i) Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inashirikiana na Taasisi zingine na vyanzo vingine vya taarifa ili kuiongezea nguvu kanzidata yake na kuweza kuwatambua wakopaji ambao hawajulikani walipo.

(ii) Mamlaka ya Bandari Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania zinaboresha uwianishaji wa kibenki katika eneo la tozo za maegesho ya meli ili kuhakikisha unafanyika kwa ufanisi na usahihi na tofauti za kimahesabu zinamalizwa kwa wakati.

(iii) Inaangalia upya muda wa uhakiki wa madeni ya wafanyakazi kwani kuendelea kuchelewesha malipo hayo kunazidisha ongezeko la madai na hivyo kuongeza mzigo kwa Serikali.

(iv) Kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iangalie namna bora ya kuepusha hasara inayoweza kupatikana kutokana na kutokukamilika kwa mradi wa Nyumba wa Golden Premier Residence. 

(v) Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kinafanya ufuatiliaji wa karibu ili mzabuni akamilishe vigezo vya mfumo ambavyo bado havijapatikana ili mfumo uanze kufanya kazi. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527