Ripoti ya CAG: MATOKEO YA UKAGUZI WA SERIKALI KUU

3.1 Utangulizi
Sura hii inawasilisha matokeo ya ukaguzi wa Serikali Kuu. Taasisi na Maeneo yaliyohusika na Ukaguzi ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania; Usimamizi wa Deni la Serikali; Udhaifu katika Malipo ya Mafao; na Ukaguzi wa Wizara, Idara, Wakala wa Serikali, Mifuko Maalumu, na Taasisi nyingine. Aidha, Sura hii inatoa mapendekezo kwa Serikali Kuu na Vyama vya Siasa.


3.2 Matokeo ya Ukaguzi wa Serikali Kuu
Ndugu Waandishi wa Habari,
Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika Ukaguzi wa Serikali Kuu. 

3.2.1 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Usimamizi wa Mapato Yatokanayo na Kodi
Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikusanya shilingi trilioni 15.38 ikilinganishwa na malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi trilioni 17.31; hivyo kuwa na nakisi ya makusanyo kwa shilingi trilioni 1.93 ambazo ni sawa na asilimia 11 ya malengo. Jumla ya makusanyo hayo haikujumlisha shilingi bilioni 18.95 ambazo ni Vocha za Misamaha ya Kodi kutoka Hazina. Hivyo, makusanyo halisi ya mwaka 2017/18 ni shilingi trilioni 15.40 yakijumuisha na Vocha za Misamaha ya Kodi kutoka Hazina.

Kodi Zilizoshikiliwa katika Kesi za Muda Mrefu kwenye Mamlaka za Rufaa za Kodi
Mamlaka ya Mapato Tanzania ina Mashauri ya Kodi ya Thamani ya shilingi trilioni 382.6 kwenye Mamlaka za Rufaa za Kodi ikiwa ni ongezeko la kiasi cha shilingi trilioni 378.2 (asilimia 8595) ikilinganishwa na shilingi trilioni 4.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17. Ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na Mashauri manne yenye thamani ya shilingi trilioni 374.7 yanayoihusu Kampuni ya Uchimbaji Madini ya ACACIA.

Kutokukusanywa kwa Mapato Yatokanayo na Kodi ya Kiasi cha Shilingi Bilioni 46.81 na Dola za Marekani Milioni 2.74 
Ukaguzi wangu ulibaini kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kukusanya mapato zaidi ya shilingi bilioni 46.81 kutoka kwa walipakodi mbalimbali. Jedwali Na. 6 linabainisha taasisi, aina za kodi, na kiasi cha fedha ambacho hakikukusanywa.

Jedwali Na. 6: Taasisi ambazo Hazikukusanya Mapato Yatokanayo na Kodi 

Udhibiti Usioridhisha wa Bidhaa Zinazopitia Nchini na Zinazosafirishwa Nje ya Nchi

Ndugu Waandishi wa Habari,
Wakati wa uhakiki wa bidhaa zinazoingizwa Nchini na Nchi jirani ili zisafirishwe kwenda Nchi nyingine, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kunipatia ushahidi kuthibitisha kuwa kodi ya shilingi bilioni 57.09 ililipwa.

Aidha, nilibaini kuwa bidhaa zilizosafirishwa kutoka Nchini kwenda Nchi nyingine zilizopaswa kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani ya shilingi milioni 649.45 ziliruhusiwa kwenda nje ya Nchi bila kukamilisha taratibu za Forodha. Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kutoa ushahidi wa nyaraka za kuthibitisha kuwa kodi stahiki zilikusanywa. 

3.2.2 Usimamizi wa Deni la Serikali
Kufikia tarehe 30 Juni, 2018, Deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 50.92, ambapo Deni la ndani lilikuwa shilingi trilioni 14.73 na Deni la nje shilingi trilioni 36.19; kiasi hiki ni ongezeko la shilingi trilioni 4.84 sawa na asilimia 10.5 ikilinganishwa na Deni la shilingi trilioni 46.08 lililoripotiwa tarehe 30 Juni, 2017.

Katika ukaguzi wangu, nilibaini masuala ya msingi yafuatayo kuhusu Deni la Serikali na usimamizi wake:
(a) Mapungufu katika usahihi wa taarifa kutokana na udhibiti wa ndani usiojitosheleza katika kuweka kumbukumbu na kutoa taarifa za Deni la Serikali.

(b) Serikali kuchelewa kulipa madeni ya Benki Kuu ya kiasi cha shilingi bilioni 212.7. Kati ya hizo, shilingi bilioni 199.79  zinatokana na riba ya nakisi ya Serikali, na shilingi bilioni 12.9 ikiwa ni sehemu ya Serikali ya gharama za kudhibiti ukwasi kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2017/18.

(c) Kutokuwapo kwa uwianishaji wa taarifa za mfumo wa malipo (Epicor) na Mfumo wa Utunzaji wa Taarifa za Deni la Taifa wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth Secretariat-Debt Record Management System – (CS-DRMS)). Hii inasababisha taarifa za fedha kutowiana na vyanzo vyake, hivyo kuhatarisha uadilifu wa taarifa za Deni la Serikali.

3.2.3 Udhaifu katika Malipo ya Mafao
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika mwaka wa fedha 2017/2018, nilikagua Majalada 2,868, ambapo Majalada 2,814 yenye jumla ya shilingi bilioni 165.44 niliyaidhinisha kwa ajili ya malipo lakini Majalada 54 niliyahoji na kuyarudisha kwa Maofisa Masuuli husika kwa ajili ya masahihisho.
Kati ya Majalada 2,868 yaliyokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mafao ya Wastaafu 295 (10.5%) yalibainika kukokotolewa kimakosa. Kati ya hayo, Majalada 172 yamebainika kuwa na ziada ya malipo ya shilingi milioni 577.32 huku Majalada 123 yakiwa na upungufu wa malipo wa shilingi milioni 294.35.

Aidha, nilibaini ucheleweshaji mkubwa wa waajiri katika maandalizi na uwasilishaji wa Majalada ya wanufaika wa mafao kwa ajili ya Ukaguzi. Ucheleweshaji huo unatokana na waajiri kutotoa kipaumbele kwenye usimamizi wa uandaaji wa mafao hivyo kuwanyima wastaafu haki yao ya kupata mafao kwa wakati.

3.2.4 Ukaguzi wa Wizara, Idara na Wakala wa Serikali, Mifuko maalumu, na Taasisi nyingine

Ndugu Waandishi wa Habari,
Nilifanya ukaguzi katika wizara na idara za Serikali 65; wakala za Serikali 33, mifuko maalumu ya fedha 16, na taasisi nyingine za Serikali 42. Nilikagua pia vyama vya siasa 14, balozi za Tanzania 41, bodi za mabonde ya maji 14 na hesabu jumuifu za taifa. Katika ukaguzi wangu, nilibaini mapungufu yafuatayo:

Udhaifu Uliobainika katika Wakala za Serikali
(a) Wakala za Serikali hazikupeleka kiasi cha shilingi bilioni 9.26 kwenda Mfuko Mkuu wa Hazina kama inavyotakiwa na Kifungu cha 11 (3) cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2001 (kama iliyorekebishwa 2016);

(b) Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) unadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 57.09 ikiwa ni riba ya ucheleweshaji wa malipo kwa wakandarasi wa ujenzi na washauri wa miradi; 

(c) Kasi ndogo ya Wakala wa Majengo Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa majengo yenye thamani ya shilingi bilioni 24.06. Jedwali Na. 7 linaainisha miradi hiyo

Jedwali Na. 7: Miradi ya TBA iliyochelewa kukamilika
(d) Baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kushindwa kuhamisha fedha zilizokuwa za tozo za wakandarasi na fedha za kodi ya zuio za kazi zenye jumla ya shilingi bilioni 6.65 kwenda Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Udhaifu katika Utengenezaji wa Vitambulisho vya Taifa Kupitia Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa (NIDA)

Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika ukaguzi wa Mamlaka ya Vitambulisho ya Taifa nilibaini kuwa kati ya watu 19,662,105 waliosajiliwa, ni vitambulisho 4,511,809 tu ndivyo vilivyotengenezwa, sawa na asilimia 23 ya idadi ya watu walioandikishwa.

Aidha, nilibaini kuwa Kampuni ya IRIS Corporation Berhad ya Malaysia (Mkandarasi) imesimamisha shughuli zote za kutengeneza vitambulisho kuanzia tarehe 14 Machi 2018. Sababu za kusimamisha zinajumuisha kutolipwa deni la mkandarasi lenye thamani ya Dola za Marekani milioni 30.18 (Shilingi bilioni 69.98), na kutoongezwa kwa muda wa mkataba kwa kipindi cha miezi kumi (10) tangu kwisha kwa muda wa mkataba wa awali, tarehe 14 Machi 2018.

Manunuzi na Usimamizi wa Mikataba
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika mapitio ya taratibu za manunuzi na usimamizi wa mikataba kwenye taasisi mbalimbali za Serikali, nilibaini mambo yafuatayo ambayo yanaleta shaka katika kufikia thamani ya fedha.
(a) Kiasi cha shilingi bilioni 4.61 kilitumika kununua bidhaa, huduma, ushauri wa kitaalamu, na kazi za ujenzi ndani ya wizara, idara, na sekretarieti za mikoa pasipo kutumia taratibu za kushindanisha wazabuni kinyume na Kanuni za 163 na 164 za Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2013.  

(b) Taasisi saba (7) zilifanya manunuzi yenye thamani ya shilingi bilioni 5.37 bila kupata vibali vya Bodi za Zabuni kinyume na Kifungu cha 35 (3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2011, na Kanuni 55 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2013.  Taasisi hizo ni:
(i) Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa;
(ii) Sekretarieti ya Mkoa wa Geita;
(iii) Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga;
(iv) Wizara ya Katiba na Sheria;
(v) Jeshi la Polisi;
(vi) Jeshi la Wananchi Tanzania; na
(vii) Ofisi ya Rais - Idara ya Kumbukumbu na Utunzaji wa Taarifa

(c) Taasisi tano (5) zilifanya manunuzi ya bidhaa, huduma, na kazi za kiasi cha shilingi bilioni 1.17 bila kuwapo kwa makubaliano ya Kimkataba na Wazabuni. Hii ni kinyume na Kanuni Namba 10 (4) ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2013. Taasisi hizo ni kama inavyoonekana katika Jedwali Na. 8

Jedwali Na. 8: Taasisi zilizofanya manunuzi bila kuwapo na Mikataba na Wazabuni.
Udhaifu katika Usimamizi wa Matumizi
Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika mapitio ya taarifa za matumizi ya fedha za umma, nilibaini dosari mbalimbali katika udhibiti wa ndani kama ifuatavyo; 
(a) Matumizi ya shilingi bilioni 4.66 yalifanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda kampuni binafsi za huduma za kisheria bila kufuata makubaliano ya mikataba; na

(b) Taasisi 20 za Serikali Kuu ziliwalipa watoa huduma mbalimbali kiasi cha shilingi bilioni 1.43 pasipo kudai stakabadhi za kielektroniki. 

Taasisi hizo ni:
1. Sekretarieti ya Mkoa wa Njombe;
2. Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi;
3. Idara ya Uhamiaji;
4. Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia;
5. Ofisi ya Waziri Mkuu-Ofisi Binafsi;
6. Idara ya Huduma za Magereza;
7. Ofisi ya Waziri Mkuu;
8. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano – Sekta ya Mawasiliano;
9. Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga;
10. Mahakama ya Tanzania;
11. Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga;
12. Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi;
13. Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi – Hospitali ya Rufaa Sokoine;
14. Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani;
15. Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro;
16. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;
17. Tume ya Maendeleo ya Usharika Tanzania;
18. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto;
19. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; na
20. Wizara ya Kilimo;

(c) Malipo yalifanyika kimakosa katika vifungu visivyostahili ya kiasi cha shilingi bilioni 885.99 kinyume na Kanuni ya 42(2) ya Kanuni za Fedha za Umma za Mwaka 2001. Jedwali Na. 9 linaonesha taasisi zilizofanya malipo kimakosa kwenye vifungu visivyostahili.

Jedwali Na. 9: Malipo Yaliyofanyika Kimakosa kwenye Vifungu Visivyostahili

Shilingi Bilioni 2.54 za Mapato Yasiyotokana na Kodi ambayo Hayakuwasilishwa Mfuko Mkuu

Ndugu Waandishi wa Habari,
Ukaguzi ulibaini kuwa kiasi cha shilingi bilioni 2.54 kilichokusanywa na Balozi 7 za Tanzania katika mwaka wa fedha 2017/18 hakikuwasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina kinyume na Kifungu cha 11 cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha ya Mwaka 2001. Badala yake, kiasi hicho cha fedha kilibakizwa katika akaunti za fedha za Balozi husika. Jedwali Na. 10 linaonesha makusanyo yaliyofanywa na Balozi, ambayo hayakuwasilishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina.

Jedwali Na. 10: Mapato Yasiyotokana na Kodi ambayo Hayakuwasilishwa Mfuko Mkuu


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post