Ripoti ya CAG: MATOKEO YA UKAGUZI WA MIRADI YA MAENDELEO

6.1 Utangulizi
Sura hii inawasilisha matokeo ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo. Maeneo yaliyohusika na Ukaguzi ni Kutorejeshwa kwa Fedha za Miradi zilizokopwa; Kodi ya Ongezeko la Thamani kulipwa kinyume na makubaliano ya Miradi; na Uchangiaji usioridhisha wa Serikali kwenye Miradi kinyume na makubaliano na Wadau wa Maendeleo. Maeneo mengine ya Ukaguzi ni Utekelezaji Hafifu wa Usambazaji wa Umeme Vijijini kupitia Mradi wa Wakala wa Nishati Vijijini; Kasi ndogo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mradi wa Uboreshaji wa Makazi; Ucheleweshaji wa kukamilika kwa Ujenzi wa Miradi ya Maji; na kutotumika kwa Mradi wa Dampo uliokamilika. 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo umebaini masuala mbalimbali ambayo Serikali inapaswa kuyafanyia kazi ili kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma. Masuala hayo yameainishwa kwa kina katika Ripoti ya Miradi ya Maendeleo, ambayo nimeiwasilisha kwako leo na muhtasari wake ni kama ifuatavyo;

6.2 Kutorejeshwa kwa Fedha za Mradi Shilingi Milioni 939.92 Zilizokopwa 

Ukaguzi wangu ulibaini kuwa Maofisa Masuuli wa miradi saba walikopa fedha za miradi jumla ya shilingi milioni 939.92 kwa ajili ya kugharimia matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2018. Fedha hizi hazikurejeshwa kwenye miradi husika na hivyo kuathiri utekelezaji wa shughuli za miradi zilizopangwa.

6.3 Kodi ya Ongezeko la Thamani ya Shilingi Bilioni 12.16 Iliyolipwa Kinyume na Makubaliano ya Miradi 

Ukaguzi wangu ulibaini kuwa malipo ya kodi ya ongezeko la thamani kiasi cha shilingi bilioni 12.16 yalifanywa na watekelezaji wa miradi 45 kinyume na makubaliano ya mikataba ya utekelezaji wa miradi husika. 
6.4 Uchangiaji wa Serikali Usioridhisha kwenye Miradi kiasi cha Shilingi Bilioni 111.01 Kinyume na Makubaliano na Wadau wa Maendeleo 

Ukaguzi wangu wa miradi mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2018 ulibaini kuwa miradi kumi ambayo Serikali ilitakiwa kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 118.44, ilichangia shilingi bilioni 7.43, sawa na asilimia sita tu. Hali hii ilisababisha upungufu wa kiasi cha shilingi bilioni 111.01 kinyume na makubaliano na wadau wa Maendeleo. Serikali kushindwa kuchangia miradi hii kwa kiasi kikubwa kumeathiri utekelezaji wa miradi husika na kudhoofisha juhudi za kufikia malengo yaliyokusudiwa.

6.5 Utekelezaji Hafifu wa Wakala wa Nishati Vijijini Kusambaza Umeme Vijijini 

Ukaguzi wa Miradi ya Nishati ulibaini kuwa Wakala wa Nishati Vijijini ilipanga kusambaza umeme kwenye vijiji vya Tanzania Bara vinavyokadiriwa kufikia 12,268 kuanzia mwaka 2013 hadi kufikia mwaka 2021. Hata hivyo, kufikia tarehe 30 Juni, 2018, mradi huo ulikuwa umefikisha umeme kwenye vijiji 4,395 tu, sawa na asilimia 36 kwa kipindi cha miaka mitano. Hali hii inaondoa uwezekano wa kufikia lengo la kusambaza umeme kwenye vijiji 7,873 vilivyobaki katika kipindi cha miaka mitatu iliyosalia hadi 2021. 

6.6 Kasi Ndogo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mradi wa Uboreshaji Makazi 

Mradi wa uboreshaji wa makazi unatarajiwa kukamilika mnamo tarehe 28 Juni, 2019. Hata hivyo, ukaguzi ulibaini kuwepo kwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijatumika cha Dola za Marekani milioni 36.25 sawa na shilingi bilioni 81.80. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 60 ya fedha za mkopo wa Dola za Marekani milioni 60 zilizotolewa kwa ajili ya mradi huu. Kuwepo kwa kiasi kikubwa cha fedha za mradi ambazo hazijatumika kumesababishwa na kasi ndogo ya utoaji wa mikopo na mchakato mrefu wa manunuzi. Hivyo, kuna uwezekano mdogo wa fedha hizi kutumika kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2019.

6.7 Kuchelewa Kukamilika kwa Ujenzi wa Miradi ya Maji

Ukaguzi wa miradi ya maji ulibaini kuwa miradi ya maji 65 inayotekelezwa na Halmashauri 22 za Mamlaka za Serikali za Mitaa yenye thamani ya shilingi bilioni 63.7 ilichelewa kukamilika kwa kipindi cha kati ya miezi 3 hadi 48. Uchelewaji huu ulitokana na uwepo wa wakandarasi wasio na uwezo; ucheleweshaji wa fedha kutoka Serikalini, changamoto za usanifu wa michoro; na mapungufu yatokanayo na manunuzi.

6.8 Kutotumika kwa Mradi wa Dampo Uliokamilika Wenye Thamani ya Shilingi Bilioni 2.96

Ukaguzi wangu ulibaini uwepo wa Mradi wa Dampo wa thamani ya shilingi bilioni 2.96 mjini Kigoma Ujiji, ambao licha ya ujenzi wake kukamilika, Dampo hilo halikuwa limeanza kutumika. Hali hii ilitokana na Ujenzi wa Shule ya Msingi karibu na mradi huo na hivyo kutumika kwa dampo lile kunaweza kuleta athari za Kimazingira kwa Wanafunzi na Miundombinu ya Shule. 

6.9 Mapendekezo

Ndugu Waandishi wa Habari, 
Ili kurekebisha kasoro nilizozibainisha katika ripoti yangu, ninaishauri Serikali ihakikishe:
(i) Fedha zilizolipwa kama kodi ya ongezeko la thamani kwenye miradi 45 iliyosamehewa kodi zinarejeshwa ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo husika. Aidha, ninashauri watekelezaji wa miradi kuzingatia mikataba ya makubaliano na wadau wa miradi ya maendeleo kwa kuhakikisha kuwa miradi iliyosamehewa kodi hailipi kodi hizo ili kusaidia kukamilika kwa wakati miradi hiyo.

(ii) Inaweka utaratibu wa uwajibikaji ili kuhakikisha fedha za miradi zinapelekwa kwa wakati na kulingana na bajeti iliyoidhinishwa ili kutokuathiri utekelezaji kwa ufanisi wa miradi hiyo.

(iii) Inaanzisha ofisi itakayokuwa na jukumu la kuratibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo nchini.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post