MTOTO ANYOFOLEWA SEHEMU ZA SIRI


Watu wawili wameuawa katika matukio tofauti wilayani Muleba mkoani Kagera kwa imani za kishirikina na kujichukulia sheria mkononi akiwemo mtoto aliyenyofolewa sehemu zake za siri. 

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kwamba mtu mmoja anashikiliwa na polisi, mkoani humo.

Alisema Aprili 17 mwaka huu, katika kijiji cha Ihunga, kata ya Kishanda, wilayani Muleba, wananchi walijichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia Colletha Frances (65) kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kumsababishia kifo na kuamua kumchoma moto nyumba yake pamoja na kufyeka mashamba ya migomba na kuyachoma.

Kamanda Malimi alisema chanzo cha mauaji hayo ni kumtuhumu Colletha kuwa ni mchawi na kumhusisha na kifo cha Ismail Hamisi (7) aliyetoweka tangu Aprili 5 mwaka huu na mwili wake kugundulika ukiwa umezikwa kwenye shamba la mama huyo umbali wa mita 60 kutoka ilipo nyumba yake, Aprili 17 mwaka huu.

Aliongeza kuwa baada ya mwili kuonekana eneo hilo wananchi walikusanyika na kuhamasishana kuvamia nyumba ya Colletha, wakamtaka atoke nje na alipotoka alikuta umati mkubwa wa watu walioanza kumshambulia na silaha za jadi hadi kumuua.

Kamanda Malimi alisema chanzo cha ukatili huo ni kumtuhumu na kifo cha Ismail kuanzia mazingira ya kupotea kwake hadi kifo na aliongeza kuwa mwili wa Ismail uligundulika kuwa umenyofolewa sehemu zake za siri.

 Alisema kuhusu tukio la mauaji ya mtoto huyo hakuna anayeshikiliwa isipokuwa katika tukio la kujichukulia sheria mkononi uchunguzi umeanza na mtu mmoja anashikiliwa kwa mahojiano zaidi, akituhumiwa kuwa mhamasishaji mkuu. Hata hivyo hakumtaja jina kwa sababu za kiuchunguzi.

Na Diana Deus, Muleba 
Na Diana Deus, Muleba 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527