ATUPWA JELA MIAKA 60 KWA KUMBAKA MTOTO AKIJISAIDIA KICHAKANI


Mahakama ya Wilaya na Mkoa wa Lindi, imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Kilangara, Abubakari Kipande (58), kifungo cha jumla ya miaka 60 jela baada ya kupatikana na makosa mawili ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 11.

Hukumu hiyo ilitolewa na mahakimu wawili tofauti, James Karyhemaa na Franco Kiswaga, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka katika kesi mbili namba 106 na 107/2018, zilizofunguliwa.

Mshtakiwa Kipande alifunguliwa kesi hizo na mlalamikaji ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili. 

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hizo, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na kuomba asipewe adhabu kali kwa kile alichodai ana familia akiwamo mke, watoto pamoja na wazazi wanaomtegemea, ombi ambalo lilitupiliwa mbali.

Baada ya utetezi huo, wanasheria wa serikali Abdurahamani Mohamedi Mshamu na Yahaya Gumbo, kila mmoja kwa wakati wake waliiomba mahakama kumpa mshtakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo.

Wakitoa hukumu katika kesi hizo, mahakimu hao, Karymaha na Kiswaga kupitia vifungu vya sheria 130 (1),(2) (e) na 131 (1) na (e) kanuni ya adhabu ya makosa sura 16 ya marejeo 2002, kwa nyakati tofauti, walipinga utetezi wake na kumhukumu kifungo cha miaka 30, katika kila kosa na kufanya aende gerezani kutumikia adhabu ya jumla ya miaka 60.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na wanasheria wa serikali Mshamu na Gumbo kuwa mshtakiwa Kipande, Februari na Agosti 13, mwaka jana, alimbaka mtoto huyo (jina linahifadhiwa) mwanafunzi wa darasa la pili.

Aidha, walidai mshtakiwa kwa mara ya pili alikamatwa na wanafunzi, wakati akifamfanyia kitendo hicho cha kinyama mlalamikaji, alipokuwa ameenda kichakani kujisaidia haja ndogo.

Wanasheria hao walisema wanafunzi hao walimfikisha mshtakiwa kwa walimu wao, ambao nao walimfikisha polisi kwa hatua kisheria.
Chanzo - Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post