MASAUNI AMVAA KATIBU WA TUME YA DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amemtaja Katibu wa Tume ya Dawa za Kulevya Zanzibar, Heriyangu Mgeni kuwa ni mmoja wa wanaokwamisha juhudi za serikali katika kupambana na dawa hizo nchini.

Akizungumza na wanahabari, April 20 viziwani Zanzibar, Naibu Waziri Masauni amesema kuwa atatoa mapendekezo kwa mamlaka inayohusika na mapambano ya dawa hizo kumwondoa katika nafasi yake kutokana na uzembe anaoufanya.

"Mimi nikiwa na dhamana, mara kadhaa nimekuwa nikimwita Katibu nikishauriana naye kwa kuwa suala la dawa za kulevya linaniumiza roho, ni mpaka leo Kisiwa cha Zanzibar chenye watu milioni 1.3 kinashindwa kupambana matatizo ya dawa za kulevya kwa kiwango kinachostahili", amesema Masauni.

"Maazimio ya kikao ilikuwa ni kushughulika na watu hao ambao Katibu alisema anawafahamu kuwa wanamkwamisha. Nilimweleza mbele ya kikao kuwa nataka unipatie data nikashughulike, naacha Bunge nakwenda Zanzibar kwa shughuli hii, siwezi kusubiri Rais John Magufuli anitumbue mimi kwasababu ya uzembe wa watu wachache", ameongeza.

Aidha Naibu Waziri huyo amesema kuwa haoni kama Zanzibar ina nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya kwa aina ya Katibu huyo aliyedai anakwamisha juhudi za serikali.

Hata hivyo amegundua kuna mapungufu ya baadhi ya askari kwa kuwa wapo wanaoharibu kesi za dawa za kulevya makusudi kwa kuchukua rushwa kutoka kwa wauzaji wa dawa hizo wanaojulikana na kuwaachia mitaani na amemwelekeza Katibu wa Wizara hiyo kuunda tume maalumu itakayokuja kufanya kazi Zanzibar kuwabaini askari wanaozorotosha jambo hilo na hatua za haraka zichukuliwe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post