MMILIKI WA SHULE YA SCHOLASTICA AGUSWA KATIKA MAELEZO YA UNGAMO ,NI KATIKA KESI YA MAUAJI YA MWANAFUNZI SHULE YA SCHOLASTICA

Na Dixon Busagaga

SHAHIDI  Irene Mushi (35)  ambaye ni wa kwanza kwenye kesi ndani ya kesi ya Msingi ya Mauaji ya kukusudia namba CC 48/2018 ya Mwanafunzi Humphrey Makundi amewasilisha Nyaraka ya Maelezo ya Ungamo ya Mshitakiwa wa kwanza katika shauri hilo ,Hamis Chacha  alivyo tekeleza agizo la Mshtakiwa wa pili ,Edward Shayo la kwenda kutupa Mtoni mwili wa mtu aliyeuawa.

Hatua ya Mahakama kujielekeza katika usikilizwaji wa kesi ndani ya kesi unatokana na mabishano ya kisheria  baina ya upande wa utetezi dhidi ya upande wa Jamhuri baada ya Upande wa utetezi kuwasilisha hoja ya kupinga kupokelewa kwa maelezo ya Ungamo katika kesi ya Msingi.

Maelezo ya Ungamo ya Mshtakiwa wa kwanza katika shauri hilo Hamis Chacha Wisare yalitolewa mbele ya Shahidi wa 14 katika kesi ya Mauaji ya kukusudia , Irene Mushi ,Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ,Moshi mjini ambaye pia ni mlinzi wa Amani .

Shauri hili linaloendelea Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ,mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ,Divisheni ya Rushwa na uhujumu Uchumi,Dar es Salaam ,Firmin Maatogoro linawakabili washtakiwa watatu ambao ni Hamisi Chacha ,mlinzi wa shule ya Sekondari ya Scholastica,Edward Shayo,mmiliki wa shule na Laban Nabiswa ,Mwalimu wa nidhamu shule ya sekondari ya Schoalastica.

Akiwasilisha kusudio la upande wa utetezi ,Wakili wa kujitegemea ,Gwakisa Sambo  aliieleza mahakama kuwa upande wa utetezi unapinga maelezo ya mtuhumiwa  na kwamba yalichukuliwa bila ridhaa yake ndipo Mahakama  ikajielekeza katika usikilizwaji wa kesi ndani ya kesi.

Akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali,Joseph Pande,shahidi Irene Mushi aliieleza Mahakama akiwa na Jukumu la Mlinzi wa Amani alipokea taarifa kutoka kwa Mfawidhi, akimueleza kwamba kuna mshtakiwa anapelekwa mbele yake kwa ajili ya kuandika maelezo ya Ungamo.

Alieleza kuwa alifuata taratubu zote na uchukuaji maelezo ya Mtuhumiwa ikiwa ni pamoja kujibu maswali tofauti ikiwemo kwa nini yupo mbele ya mlinzi wa amani na endapo maelezo atakayotoa yataenda kutumika kama sehemu ya ushahidi endapo atafikishwa Mahakamani huku majibu yake yakiwa anafahamu.

Alieleza kuwa mtuhumiwa alikuwa katika Afya nzuri na kwamba aliimuliza endapo kama alipigwa ama kutishiwa alimjibu alipigwa tarehe 17/11/2017 na askari Polisi baada ya maelezo yake kutofautiana na y a mlinzi mwenzake.

Baada ya maelezo hayo Wakili Mkuu wa Seriali ,Joseph Pande alimuonesha karatasi ya maelezo ya mshtakiwa na kuuliza kama anaitambua alijibu ndio na kuiomba mahakama kuitumia kama kielelezo katika ushahidi wake na kupokelewa baada ya kuridhiwa na pande zote mbili.

Baada ya kielelezo hicho kupokelewa Shahidi Irene akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali anaye wakilisha upande wa Jamhuri katika Shauri hilo alielekezwa kusoma maelezo yaliyoandikwa katika nyaraka ya maelezo ya ungamo katika mahakama ya mwanzo Moshi mjini.

Katika sehemu ya maelezo ya Shahidi huyo wakati akisoma maelezo ya Ungamo ya Mshtakiwa Hamisi Chacha ,Shahidi huyo alieleza kwamba  Chacha akiwa eneo lake la kazi alisikia kishindo cha mtu ndipo alipoamua kupiga tochi na kufuatilia baada ya kubaini kuwa kuna mtu .

Ameileza mahaka kuwa Mtuhumiwa alimueleza kuwa alimpiga mtu huyo na  bapa la Panga  na akaumia kenye  paji la uso  na baadae akampiga bapa la pili  na mtu alifariki pale pale ndipo alipompigia simu Mwalimu Laban aliyefika eneo hilo na kusema huenda mtu huyo amezirai.

Alieleza Labani aliiuliza kama ameshafanya mawasiliano na Mzee Shayo  na baadae alipigiwa Shayo ambaye anatajwa kama mmiliki wa shule hiyo aliyefika eneo la tukio na kutoa maelekezo ya mtu huyo kwenda kutupwa mtoni kama hafahamiki na kwamba huenda ni Kibaka.

Irene ameeleza baada ya hapo yeye Chacha na Mwalimu  Labani wakauchukua ule mwili wa marehemu wakaenda kuutupa mtoni na kurudi shuleni na kuitisha Row call kwa ajili ya kujua endapo kama ni mwanafunzi  hayupo  shuleni .

 Shahidi alieleza Mlinzi Chacha alielekea kwenye  Mabweni  na kukuta kitanda kimoja  hakina mwanafunzi na Mwalimu  Laban aliuliza ni mwanafunzi gani hayupo ,baade ilibainika kuwa mwanafunzi Humphrey Makundi wa kidato cha pili ndio hayupo.

Upande wa Jamhuri unaaongozwa na Wakili Mkuu w Serikali ,Joseph Pande ,Wakili wa serikali Mwandamizi,Abdalah Chavula,Wakili wa Serikali ,Omari Kibwana na Wakili wa serikali ,Lucy Kiusa waliieleza mahakama kuwasilisha mashahidi wa nne.

Upande wa utetezi  ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea ,Elikunda Kipoko anaye mtetea Mshtakiwa wa pili ,Edward Shayo akisaidiana na Wakili wa kujitegemea Gwakisa Sambo, Wakili wa kujitegemea David Shilatu anaye mtetea Mshitakiwa wa kwanza ,Hamis Chacha na Wakili wa kujitegemea Patrick Paul walieleza mahakama watawaasilisha shahidi mmoja ambaye ni Hamisi Chacha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post