Picha : AGAPE YATOA ELIMU YA AFYA YA UZAZI NA UJINSIA KWA VIJANA KWA NJIA YA MICHEZO...ZAWADI NONO ZATOLEWA KWA WASHINDI

Shirika la Agape AIDS Control Programme limetoa elimu ya afya uzazi na ujinsia kwa vijana kwa njia ya michezo katika kijiji cha Manyada kata ya Usanda Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ili kukabiliana na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,mimba na ndoa za utotoni pamoja na ukatili wa kijinsia. 

Elimu hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 5,2019 katika Uwanja wa Kitongoji cha Mwagala ambapo michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu,kukimbiza kuku na mbio za baiskeli kwa wanaume na wanawake imefanyika ikihusisha vijana walio nje ya shule. 

Washindi katika michezo hiyo kutoka vitongoji vya Buchamike,Mwagala,Uswahilini,Sagabahi na Munge wameondoka na zawadi ikiwemo kuku na mbuzi huku wakipata ujumbe wa aina mbalimbali kuhusu namna ya kulinda afya zao lakini pia kutokomeza mimba na ndoa za utotoni na ukatili dhidi ya wanawake katika jamii. 

Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga alisema elimu hiyo inatolewa kwenye maeneo ya pembezoni ‘Hard to reach communities’ katika kata ya Usanda ili jamii ichukue tahadhari kuhusu maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa na kutokomeza mimba na ndoa za utotoni. 

“Michezo hii imeshirikisha vijana ambao wapo nje ya shule,tunaamini elimu hii itawasaidia vijana ikizingatiwa kuwa vijana ndiyo wapo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU na vijana hawa ndiyo wamekuwa wakiwatia mimba watoto na kuwakatisha masomo shuleni”,alieleza Maganga. 

Akitoa elimu ya afya,Muuguzi kutoka Kituo cha Afya Usanda,Jesca Mabula aliwahamasisha vijana kufanyiwa tohara kwani inakinga kwa asilimia 60 dhidi ya maambukizi ya VVU na kutumia kondomu huku akiwashauri kupima afya zao ili kubaini kama wana maambukizi ya VVU au la. 

Pia aliwataka wanaume kuachana na tabia ya kuchepuka pindi wake zao wanapojifungua kwani kitendo hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa. 

“Wanaume tunzeni wake zenu,acheni kuchepuka na kuuza vyakula kwa ajili ya kuwahonga na hata kuoa wanawake wengine,pia muwaruhusu wake zenu kupanga uzazi wa mpango na muwe na tabia ya kutembelea vituo vya afya kwa ajili ya ushauri kuhusu masuala ya afya”,alieleza. 

Muuguzi huyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wazazi na walezi juu ya umuhimu wa kukaa karibu na watoto wao wa kike na kuwaeleza kuhusu mabadiliko ya mwili na kuhakikisha wanawapeleka shule badala ya kuwaozesha wangali wapo katika umri chini ya miaka 18.

Shirika la Agape la mkoani Shinyanga linatekeleza mradi wa afya ya uzazi na ujinsia katika kata ya Usanda kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Sida nchini Sweden kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii ili kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni,maambukizi ya VVU na ukatili wa kijinsia.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO KUTOKA UWANJANI
Mgeni rasmi, Afisa Mtendaji kata ya Usanda,Emmanuel Maduhu akizungumza wakati Shirika la Agape likitoa elimu ya afya uzazi na ujinsia kwa vijana kwa njia ya michezo katika kijiji cha Manyada kata ya Usanda Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa Mtendaji kata ya Usanda,Emmanuel Maduhu akiwasisitiza vijana kufanyiwa tohara pamoja na kuachana na tabia ya kuuza vyakula na kwenda kuhonga wanawake wageni wanaofika eneo hilo 'malaya' na kuwataka wananchi kuachana na tabia ya kuozesha watoto badala yake wawapeke shule wakasome.
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga akiwahamasisha wananchi kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kukabiliana na maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa,kutokomeza mimba na ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia. 
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga akiwataka wananchi kutowaozesha watoto.
Muuguzi kutoka Kituo cha Afya Usanda,Jesca Mabula akitoa elimu ya afya ya uzazi na kuwashauri vijana kujitokeza kufanyia tohara na kuwahamamisha kutumia kondomu na kuachana na michepuko watunze wake zao.
Muuguzi kutoka Kituo cha Afya Usanda,Jesca Mabula akiendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Muuguzi kutoka Kituo cha Afya Usanda,Jesca Mabula akiwataka akina mama kuacha tabia ya kupeleka watoto wao wa kike kwa waganga wa jadi kutafuta dawa ya kupendwa 'samba' ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni pamoja na maambukizi ya VVU.
Afisa Miradi wa shirika la Agape, Mustapha Isabuda akiwasisitiza vijana wafanyiwe tohara na kuacha kutamani watoto wa shule kuhusu akiwashauri wanaume wanaopenda watoto wa shule wawashonee sketi za shule wake zao ili tamaa ya kutamani watoto wa shule.
Ukafika wakati wa michezo : Pichani ni washiriki wa mbio za baiskeli wakichuana vikali katika uwanja wa kitongoji cha Mwagala kijiji cha Manyada kata ya Usanda.
Washiriki wa mbio za baiskeli wakichuana vikali katika round 20 kuzunguka uwanja ambapo mshindi wa kwanza alipata zawadi ya mbuzi mmoja.
Ni burudani tu!! Vijana wa kike hawakuwa nyuma katika mbio za baiskeli wakichuana vikali...Hapa wanaoneshana nani mkali katika round 5 kuzunguka uwanja.
Mshindi wa kwanza upande wa vijana wa kike Juke Jackson akimaliza mchezo.
Vijana wa kike wakijiandaa kukimbiza kuku.
Mchezo wa kukimbiza kuku ukiendelea ambapo aliyefanikiwa kukamata kuku,ndiyo ilikuwa zawadi yake...kama atakwenda kumfanya kitoweo  ama kumfuga basi kazi kwake!!

Elizabeth Masanja ndiye alifanikiwa kumkamata jogoo huyo!!
Kikosi cha timu ya mpira wa miguu Mwagala kikiwa tayari kabisa kukabiliana na timu ya  Buchamike katika uwanja wa Mwagala.
Kikosi cha timu ya mpira wa miguu Buchamike kikiwa tayari kabisa kuwavaa Mwagala.

Afisa Miradi wa shirika la Agape, Mustapha Isabuda akisalimiana na wachezaji wa timu ya Mwagala na kuwatakia mchezo mwema dhidi yao na Buchamike.

Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape, Lucy Maganga akisalimiana na wachezaji wa timu ya Mwagala.
Mchezo kati ya Mwagala na Buchamike ukiendelea.
Mchezo unaendelea....Hata hivyo Buchamike waliibuka washindi kwa kuwachapa Mwagala bao 1 - 0.
Wakazi wa kijiji cha Manyada wakishuhudia mpambano kati ya timu ya Buchamike na Mwagala.
Mchezo unaendelea.
Mashabiki wa timu ya Mwagala wakiwa uwanjani.
Wakazi wa Manyada wakishuhudia mchezo kati ya Mwagala na Buchamike.
Wananchi wakiwa uwanjani.
Mashabiki wa timu ya Buchamike wakishangilia baada ya timu yao kuwachapa Mwagala bao 1 - 0
Mshereheshaji Mkuu, Victor Komba ambaye ni mwalimu kutoka shule ya msingi Shabuluba akitoa mwongozo wa ugawaji zawadi kwa washindi kwenye michezo iliyofanyika uwanjani.
Mgeni rasmi, Afisa Mtendaji kata ya Usanda,Emmanuel Maduhu (kushoto) akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa mshindi wa kwanza shindano la mbio za baiskeli upande wa wanaume Jeremiah Dotto.
Mgeni rasmi, Afisa Mtendaji kata ya Usanda,Emmanuel Maduhu akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa mshindi wa kwanza shindano la mbio za baiskeli upande wa wanawake Juke Jackson (aliyebeba mtoto).
Washindi wa pili shindano la mbio za baiskeli (Emmanuel Malale upande wa wanaume na Mariam Segese upande wa wanawake) wakiwa wamebeba zawadi ya kuku baada ya kukabidhiwa.
Mgeni rasmi, Afisa Mtendaji kata ya Usanda,Emmanuel Maduhu akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa mwakilishi wa timu ya Mwagala ambao ni washindi wa pili katika mchezo wa mpira wa miguu baada ya kufungwa bao 1-0 na timu ya Buchamike.
Afisa Mtendaji kata ya Usanda,Emmanuel Maduhu (kushoto) akikabidhi zawadi ya mbuzi wawili kwa washindi wa kwanza shindano la mpira wa miguu (Buchamike).
Golikipa wa timu ya Buchamike Ntalike Juma(kushoto) na Kapteni wa timu hiyo Jimogela Mwita wakibeba zawadi ya mbuzi wawili.
Golikipa wa timu ya Buchamike Ntalike Juma(kushoto) na Kapteni wa timu hiyo Jimogela Mwita wakiondoka na zawadi ya mbuzi wawili.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527