Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ametetea msaada na ushirikiano wa nchi hiyo na Saudi Arabia katika vita vyake dhidi ya watu wa Yemen kwa kudai kuwa jambo hilo ni lenye maslahi makubwa kwa Marekani.
Mike Pompeo alitoa matamshi hayo jana Jumatatu akiashiria mashambulio ya makombora ya kulipiza kisasi yanayovurumishwa na harakati inayopendwa sana nchini Yemen ya Ansarullah, ambayo imekuwa ikitetea na kuilinda nchi hiyo kutokana na uvamizi wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Ansarullah imekuwa ikilenga na kuvishambulia vituo na taasisi muhimu za kistratijia za Saudia ili kuizuia nchi hiyo kuendeleza mashambulio yake hayo ya kivamizi dhidi ya taifa la Yemen.
Marekani, Israel na Uingereza zimekuwa zikiipa msada mkubwa wa kijeshi Saudi Arabia na washirika wake tokea waivamie Yemen mwezi Machi mwaka 2015.
Msaada na ushirikiano huo wa Washington na Riyadh umekuwa ukikosolewa vikali ndani ya Marekani na hasa katika Kongresi ya nchi hiyo kufuatia kuuawa kinyama kwa Jamal Khashoggi, mwandishi na mkosoaji mkubwa wa utawala wa kidhalimu wa Saudi Arabia, huko Istanbul Uturuki, mwezi Oktoba mwaka uliopita.
Mapema mwezi huu, Rais Donald Trump wa Marekani alipinga kwa veto mswada uliopitishwa na Kongresi hiyo kwa ajili ya kusimamishwa ushirikiano na msaada huo wa kijeshi wa Marekani kwa Saudia.
Vita hivyo vimepelekea zaidi ya Wayemen 70,000 kupoteza maisha yao ambapo 10,000 kati yao waliuawa katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.
Vita hivyo pia vimeharibu pakubwa miundombinu ya nchi hiyo zikiwemo hospitali, shule, viwanda na barabara. Umoja wa Mataifa tayari umeonya kwamba Wayemen milioni 22.2 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na kwamba milioni 8.8 kati yao wanakabiliwa na hatari ya janga la njaa. Kwa mujibu wa ripoti ya umoja huo, Yemen inakabiliwa na janga kubwa zaidi la njaa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.