Picha : MVUA KUBWA YASABABISHA MAFURUKO KAHAMA MJINI,...NI BALAA


Mvua kubwa iliyonyesha leo asubuhi Aprili 26,2019 katika maeneo mbalimbali wilayani Kahama mkoani Shinyanga imesababisha baadhi ya nyumba katika mitaa ya Malunga, Mhongolo na Sokola mjini Kahama kujaa maji na kuharibu vitu mbalimbali vilivyokuwa ndani.

Wananchi wameshuhudiwa na mwandishi wetu, wakiendelea kutoa maji katika makazi yao kwa kutumia ndoo huku Jeshi la Zima moto na uokozi nalo  likiendelea na kazi ya kuokoa wenye uhitaji.

Baadhi ya wananchi wamesema idadi kubwa ya watoto wameokolewa na kupelekwa kwenye makazi mengine yenye mwinuko na kwamba usalama wao upo hatariani na kuishauri serikali kuboresha miundombinu ya mitaro na madaraja.

Diwani wa Kata ya Mhongolo ambaye ameshiriki kuokoa baadhi ya watoto Michaele Mizubo amesema nyumba nyingi zimejaa maji na kwamba ameelekeza walioathirika na mvua hiyo wapewe hifadhi ya makazi ya muda huku akishauri ujenzi wa barabara unaoendelea ni vyema kuwa wanawashirikisha viongzi wa mitaa na kata.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, wilayani Kahama Thomas Muyonga ambaye amefanya ziara katika eneo hilo amewataka wanachi kuendelea kuchukua tahadhari na kuwataka kutozua njia ya maji na wataishauri serikali kuona inaweka nguvu katika eneo hilo ili kuondoa adha hiyo.

Maeneo mengine ambayo wananchi wamedai kuathiriwa na mvua hiyo ni pamoja na Kitongoji cha Maliasili cha Mtaa wa Nyahanga, Igomelo, Mayila Nyihogo, na Sango Nyasubi ambapo maji yameingia kwenye makazi yao pamoja na kuharibu miundombinu ya barabara.

Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha amesema  hakuna mtu aliyeripotiwa kupoteza maisha na kwamba maeneo yaliyoathirika ni yale ambayo yalikuwa yanatumika kwa kilimo cha mpunga na baadae wananchi walianza kujenga nyumba hivyo walijenga wenyewe kwenye mkondo wa maji.

Na Kijukuu Blog Kahama
Nyumba zikiwa zimezingirwa na maji
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post