MWALIMU ATUPWA JELA MIAKA 30 KWA KUMBAKA MWANAFUNZI WAKE NDANI YA SALUNI SIMIYU

Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, imemhukumu Mwalimu Abubakari Katakweba (32) wa Shule ya Msingi Mwafa wilayani humo, kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Fredrick Lukuna, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kutoa adhabu hiyo.

Hakimu Lukuna alisema mashahidi wote waliofika mbele ya mahakama hiyo walieleza jinsi mshtakiwa huyo ambaye ni mwalimu alivyofanya kitendo hicho, ikizingatiwa ni mlezi au mzazi wa wanafunzi wote.

Hata hivyo, mshtakiwa baada ya kutiwa hatiani, aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ndilo kosa lake la kwanza na pia ana familia ambayo inamtegemea.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, Nassib Swedy, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 10,mwaka huu katika Kijiji cha Hinduki wilayani humo.

Mwendesha Mashtaka Nassib alieleza mahakama hiyo kuwa siku ya tukio saa 1:00 jioni, mshtakiwa akiwa katika eneo lenye vibanda vya biashara katika kijiji hicho, alimwita mwanafunzi huyo wa Shule ya Sekondari Sukuma.

Alisema kwa kuwa mwanafunzi huyo alimfahamu mshtakiwa kuwa ni mwalimu, alikwenda lakini ghafla alimshika mkono na kisha kumfumba mdomo kwa mkono wake ili asipige kelele na kumwingiza katika chumba ambacho kilikuwa kikitumika kunyolea nywele (saluni) na kisha kumvua nguo na kuanza kumbaka.

Mwendesha mashtaka huyo alisema kitendo hicho ni kinyume na kifungu 130(1)(2) na kifungu 131(1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527