SERIKALI YAFUNGUKA KUHUSU DAWA ZA KUONGEZA NGUVU ZA KIUME NA MAKALIO


Suala la matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu za kiume na makalio limeibuka bungeni huku Waziri wa Ulinzi, Dkt.Hussein Mwinyi akiwataka watanzania wanaotaka kutumia huduma hiyo kufuata taarifa rasmi kabla ya matumizi.

Awali swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Rukia Kassim ambaye alihoji juu ya Serikali kuzifungia saluni ambazo zinatoa huduma ya kutumia dawa na kuongeza makalio na kubandika kucha bandia.

"Wanawake wengi wameathirika sana kwa dawa za kuongeza makalio, kope na kucha bandia, je Serikali iko tayari kuzifunga saluni zinazofanya hivi?", aliuliza Mbunge huyo.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Wizara ya Afya, Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema, "TFDA haijawahi kupokea taarifa ya madhara kuhusiana na kucha za kubandika, kukosekana kwa takwimu hizo Serikali haina sababu ya kufunga saluni, wala kuwachukulia hatua watoa huduma".

Kwa upande wa Mbunge wa Ulanga Goodluck Mlinga, aliyehoji juu ya kuongezeka kwa matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume hususani kwa vijana.

"Tunatambua kuna dawa maalum zilizopitishwa kwa ajili ya kuongeza nguvu za kiume, ushauri wetu ni kwamba wanaotaka kutumia dawa hizi, wakatumie dawa ambazo zimethibitishwa na wataalam ambazo hazina madhara", amesema Waziri Mwinyi alipokuwa akijibu swali la Mbunge Mlinga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527