ASASI 65 ZA KIRAIA ZAMTAKA MSAJILI AACHE KUINGILIA MIGOGORO YA NDANI YA VYAMA VYA SIASA

Asasi 65 za Kiraia zimemtaka Msajili wa vyama vya Siasa Nchini aache kuvitisha na kuingilia migogoro ya ndani ya vyama vya siasa.

Aidha, badala yake wamemtaka aongozwe zaidi na hekima katika kusimamia misingi ya demokrasia na haki za wananchi kujiunga na vyama wanavyovitaka bila kuwekewa vikwazo visivyotambulika na sheria za nchi.

Wito huo umetolewa leo na Jukwaa la Wakurugenzi wa AZAKI katika ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC), ambapo pia zimewataka viongozi waheshimu sheria za nchi na katiba kwa kuacha kuzuia mikutano ya siasa ya ndani na nje.

Akitoa tamko kwa niaba ya Azaki hizo, kuhusu hali ya demokrasia, haki ya kujumuika na kujiunga na vyama vya siasa, Onesmo Olengurumwa kutoka THRDC, amesema kumekuwa na matukio yanayoashiria ukiukwaji wa haki za kidemokrasia haki ya uhuru wa kukifanyika na kujiunga na vyama vya siasa.

“Kama Watanzania wenye jukumu kikatiba kulinda mshikamano, umoja,haki na amani ya nchi tumeona ni vyema kuzungumza na kuwashauri viongozi wetu wa kisiasa kufuata sheria za nchi.

“Tumeshuhudia ukiukwaji wa haki hizo za kisheria na Katiba ya nchi ya mwaka 1977 na kwa kuwa asasi tumekuwa washauri na wakosoaji na wasaidizi wakubwa wa mambo mengi yakitaifa ni busara zaidi kulisemea hili ili kuhakikidha ukiukwaji wa haki hizi tajwa haziwezi kuwa sababu ya kupelekea kupoteza amani na umoja wa kitaifa,” amesema Olengurumwa.

Amesema mwenendo wa muda mrefu wa Msajili wa vyama vya Siasa kuonekana kuchukua upande katika mgogoro wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF) na kusahau yeye ni mlezi wa vyama alipaswa kutokuwa sehemu ya mgogoro ndani ya vyama.

Naye mwakilishi kutoka LHRC, Felister Mauya, amesema serikali inatakiwa kuhakikisha uhuru wa kujumuika ikiwa ni pamoja na uhuru wa kufanya maandamanao ya amani unaheshimiwa na kulindwa na vyombo vya usalama kama sheria zinavyoelekeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post