Picha : MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE SHINYANGA VIJIJINI..MBUNGE AZZA AWAKOMALIA WANAWAKE KUGOMBEA NAFASI ZA UONGOZI


Mbunge wa viti maalumu mkoa wa  Shinyanga Azza Hamad Hilal amewataka wanawake mkoani hapa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, pamoja na uchaguzi mkuu ujao (2020).


Azza amebainisha hayo leo Machi 8, 2019 kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake dunia yaliyo fanyika ki wilaya kwenye Kata ya Lyabukande halmashauri ya wilaya ya Shinyanga(Vijijini) huku yakihudhuriwa pia na mashirika mbalimbali yanayojihusisha na shughuli za maendeleo ikiwemo kupinga matukio ya ukatili ndani ya jamii.

Alisema wanawake wana uwezo mkubwa wa kuongoza jamii, na kutolea mfano wa makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan namna anavyochapa kazi katika kuwatumikia watanzania kutatua matatizo yao hivyo  kuwataka wajitokeze kwenye uchaguzi wa mwaka huu wa Serikali za mitaa  kuwania uongozi.

“Halmashauri hii ya wilaya ya Shinyanga ina jumla ya vijiji 126, lakini viongozi Wanawake ambao ni wenyeviti wapo wawili tu, hii ni aibu hivyo nawasihi wanawake wenzangu tujitokeze kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa mwaka huu na hata uchaguzi mkuu ujao mwakani,”amesema Azza.

“Halafu ukiangalia sisi wanawake tupo wengi na ndiyo wapiga kura, kwanini tusipeane sisi wenyewe nafasi za uongozi isipokuwa kwa kuangalia mtu ambaye anafaa kuwa kiongozi, ili tupate kuonyesha kuwa wanawake tunaweza kuwa viongozi wazuri,”ameongeza.

Pia aliwataka wanaume kuwaunga mkono wanawake kwa kuwapigia kura hasa pale wanapomuona anafaa kuwa kiongozi bora, na kuondoa dhana ya mfumo dume kwa kuwaona ni viumbe dhaifu na hatimaye kuacha kuwachagua.

Katika hatua nyingine Azza alikemea tabia ya wanawake wilayani humo kwenda kukopa mikopo ya halmashauri fedha za mapato ya ndani asilimia 10 na kuanza kuzitumia kwa malengo ambayo hayakukusudiwa, hali ambayo inawafanya kuendelea kuwa maskini na tegemezi katika familia zao.

Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Shinyanga Ngasa Mboje, aliwataka wanaume kuacha tabia ya kunyanyasa wanawake, huku akiahidi halmashauri itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake ikiwapo na utoaji wa fedha za mikopo kwa wingi.

Kwa upande wa risala ya wanawake wilayani humo ikisomwa na Lucy Fabiani, ilitaja baadhi ya changamoto ambazo wanakabiliana nazo, kuwa ni ukosefu wa fedha za mikopo ya kutosha, kubakwa, pamoja na kubaguliwa kwa  kutopewa nafasi za kuwania uongozi kwenye chaguzi mbalimbali.

Aidha kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani inasema "Badili fikra ili kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu", ambapo maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI


Mbunge wa Viti maalumu Azza Hamad Hilal akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika kwenye Kata ya Lyabukande na kuwataka wanawake wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mbunge wa Viti maalumu Azza Hamad Hilal  akiwasalimia wananchi waliohudhuria maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, akiwataka wanaume kuacha tabia ya kuwafanyia ukatili wanawake, bali waishi nao vizuri pamoja na kuwapenda.

Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Deus Mhoja akikemea vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na kusema vipigo kwao iwe mwisho.

Diwani wa Viti maalumu halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Yunis Magesa akizungumza kwenye siku ya wanawake duniani na kumpongeza mbunge Azza Hilal kwa kutatua changamoto ya huduma za kiafya ikiwamo kusambaza vitanda vya kujifungulia akina mama kwenye hospitali.

Lucy Fabiani akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kubainisha baadhi ya changamoto ambazo zinawakabili ikiwamo kubakwa, kutelekezewa watoto na waume zao, kukosa fedha za mikopo ya kutosha ,kunyanyaswa kupewa mirathi pamoja na kunyimwa nafasi za uongozi ndani ya jamii.

Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilal, akionya wazazi kuacha tabia ya kuozesha wanafunzi ndoa za utotoni pamoja na wanaume kuacha tabia ya kuwapachika ujauzito na kukatisha masomo yao, bali wawache watimize malengo yao.

Wanawake wa kata ya Lyabukande wakiwa kwenye  maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Shinyanga.

Wanawake wakisikiliza ujumbe mbalimbali kutoka kwa viongozi wa serikali na mbunge wa Viti maalumu Azza Hamad Hilal kwa kutakiwa kujitokeza kugombea uongozi kwenye chaguzi zijazo, pamoja na kujiunga kwenye vikundi na kuitumia mikopo kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Wanawake wakiwa kwenye siku ya maadhimisho yao.

Maadhimisho ya siku ya wanawake yakiendelea.

Maadhimisho ya siku ya wanawake yakiendelea katika kata ya Lyabukande wilaya ya Shinyanga.

Maadhimisho ya siku ya wanawake yakiendelea.

Vijana wakike wakiwa kwenye madhimisho ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Shinyanga katika kata ya Lyabukande.

Wanawake wakifurahia jambo.

Wanaume nao hawakuwa nyuma kushiriki maadhimisho hayo ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Shinyanga na kutakiwa kuacha kuwafanyia ukatili wanawake vikiwamo vipigo na kuendekeza mfumo dume.
Mwenyekiti wa wazee mkoa wa Shinyanga Faustine Sengerema ,akipinga vitendo vya mauaji ya vikongwe hasa wanawake kwa kisingizio cha ushirikina.

Awali Wadau wa maendeleo mkoani Shinyanga kutoka mashirika mbalimbali wakijitambulisha kwenye maadhimisho hayo ya wanawake duniani yaliyofanyika kiwilaya kwenye Kaya ya Lyabukande, likiwamo Shirika la Agape, Thubutu Africa Initiative, Rafiki SDO, Tawlae, PAWWCO pamoja na World Vision.

Wanawake wakiwa kwenye banda la kupima VVU 

Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilal (kushoto( akiwa na Diwani wa Viti maalumu halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Yunis Magesa, wakifurahia jambo kwenye maadhimisho hayo ya siku ya wanawake.

Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilal, akicheza nyimbo na wanawake kwenye maadhimisho hayo.

Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilal akicheza ngoma ya Kisukuma ya Waswezi.
Ngoma ya Waswezi ikiendelea kuchezwa.

Awali Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilal akiwasili kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani wilaya ya Shinyanga yaliyofanyika kwenye Kata ya Lyabukande akipokewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje.

Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilali mkono wa kushoto,akisumbili kupokea maandamano ya wanawake, katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, akifuatiwa na Afisa Elimu Sayansi Kimu wa halmashauri hiyo Merry Maka.

Jeshi la Jadi Sungusungu nalo likishiriki maandamano ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani katika Kata ya Lyabukande wilaya ya Shinyanga na kupinga matukio ya ukatili dhidi ya wanawake.

Wanawake wakiandamana wakiwa na mabango yenye jumbe mbalimbali za kupinga matukio ya ukatili dhidi yao.

Mbunge wa Viti maalumu mkoa wa Shinyanga Azza Hamad Hilal, akicheza nyimbo zenye ujumbe wa akina mama mara baada ya kumaliza kuadhimisha siku ya wanawake duniani wilaya ya Shinyanga iliyofanyika kwenye Kata ya Lyabukande.

Na Marco Maduhu- Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post