HAYA NDIYO MADHARA YA USHOGA

“Ushoga siyo kitu kigeni kwa baadhi ya jamii ya watu hapa duniani. Kilicho kigeni ni ushoga uliorasimishwa, yaani ule unaotungiwa sheria za kuwatambua na kuwalinda mashoga yaani, ushoga unaodai kuzuia kunyanyapaliwa, na kudai haki ya mashoga kuishi pamoja kama wanandoa.”


Ndivyo anavyosema Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania, Emil Hagamu akipinga vitendo vya ushoga na harakati za kuunga mkono au kutetea vitendo hivyo zinazofanywa na watu waliokengeuka kimaadili wakidai kutungwa kwa sheria ili kuwalinda mashoga.

Kimsingi, vitendo vya ushoga ni kosa la jinai nchini Tanzania kama yalivyo makosa mengine. Sheria za Tanzania haziruhusu ushoga na hii imeainishwa katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.

Hagamu anasema: “Sote tunaelewa kuwa hakuna uzao unaotokana na muunganiko wa mashoga. Mwanamume akimwoa mwanamume mwenzake, au mwanamke akimwoa mwanamke mwenzake; au kama nchi zinahimiza vitendo vya ngono baina ya watu wa jinsi moja, ni wazi, hapatakuwa na uzao.”

Kwa kadiri makundi ya mashoga yanavyoimarika katika nchi yoyote, ndivyo hivyo nchi inapungukiwa na uzao wa watoto.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa Prolife, Rais wa nchi moja barani Afrika aliwahi kushinikizwa aukubali ushoga nchini mwake kama sharti la kupatiwa misaada ya kimaendeleo.

Aliwajibu hivi waliomshinikiza: “Sizuii ushoga wala mashoga, ushoga unaweza kuwepo, na mshoga wanaweza kuoana, lakini nataka nione mimba baada ya miezi 6. Kama sitaziona mimba, basi sitaki kusikia habari za ushoga wala mashoga. Ni ujinga na upumbavu”.

Washinikizaji walikasirika sana kwa jibu hilo. Lakini ndilo jibu sahihi.

Ni upuuzi kuendekeza nadharia kengeushi na potofu za ushoga wakati tunaelewa fika kuwa zinadidimiza uzao na utu wa mtu huku ukienda kinyume na mpango wa Mungu katika uumbaji sambamba na madhara mbalimbali.

Madhara ya kisaikolojia Inaelezwa kutoka vyanzo mbalimbali kuwa, watu wengi wanaojihusisha na vitendo vya ushoga wapo hatarini kukumbwa na madhara ya kisaikolojia yakiwamo ya kufikiria na kuamua kujiua.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ya akili, wanaume anaojihusisha na mambo ya ushoga ni rahisi kupata ugonjwa wa sonona, kupata magonjwa ya zinaa, kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia na kubwa zaidi, kufikiria kujiua.

Mwanasaikolojia Tiba kutoka Kituo cha Afya cha Somedics Polyclinic cha Upanga jijini Dar es Salaam, Saldin Kimangale anasema mtu anayejihusisha na ushoga anaweza kupata matatizo makubwa kisaikolojia.

Anasema hii ni kutokana na ukweli kuwa, mashoga hasa wale wa waliojifunza ni rahisi kupata magonjwa ya akili pamoja na magonjwa mengine, lakini pia ni rahisi kwao kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya na kufanya maamuzi ya kujiua.

“Hii ni kwa sababu wanafanya vitendo ambayo ni kinyume na maumbile yao hivyo mara nyingi wengi wanalazimika kutumia Inaendelea Uk. 1pombe kupita kiasi, na pengine dawa za kulevya ili wafanye watakavyo bila hofu wala aibu kwa jamii,” anasema Kimangale.

Hata hivyo anasema: “Wale waliozaliwa hivyo, wanaweza wasiingie huko kwa sababu wao wanajiona wako sawa tu, lakini ili wapoteze mawazo wanaweza kutumia vilevi, na hatari kubwa wanaweza hata kuwa waraibu.”

Anasema kiwango cha watu wanaofanya vitendo vya ushoga kujiua au kujifanyia ukatili wowote ni mara nane zaidi ya mtu wa kawaida, hivyo mtu mwenye tabia ya ushoga anaweza kufanya maamuzi ya kujiua au kujidhuru kwa namna yoyote.

Aidha, mwanasaikolojia huyu anasema kuwa kati ya mambo yanayowasumbua watu hawa ni kutengwa, kunyanyapaliwa, kutendewa ukatili na kukataliwa kuanzia ndani ya familia zao kutokana na tabia yao hiyo isiyokubalika katika jamii za Waafrika na kwingineko duniani.

Mtaalamu huyo wa saikolojia anasema: “Watu hawa kwanza hutengwa, kunyanyapaliwa kwa kukosa huduma mbalimbali, kutendewa ukatili ukiwepo ule wa kihisia na kukataliwa kuanzia ndani ya familia zao na wengine kulazimika kuondoka nyumbani kwao kwa sababu hawakubaliki.”

Anasema mashoga wako katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa sonona kwa kuwa huishi na huzuni kwa muda mwingi katika maisha yao huku wakiwa wamepoteza matumaini. “… hujitenga na watu, hukosa usingizi na pia hupoteza hamu ya kula na hata kupata fikra za kujiua na wengine hata kujaribu kujiua kwa kuwa hawaoni thamani yao wanapoishi katika mazingira wanayopingwa kutokana na matendo yao,” anasema mtaalamu huyo.

Anasema mbali na hayo, athari hizo za kisaikolojia pia zinaweza kumsababishia shoga athari za kiafya kama kupata maradhi.

Anakwenda mbali na kusema kuwa, wapo baadhi ya mashoga wanaopambana na hali hiyo kwa kuwa hawaipendi, hasa waliozaliwa katika hali hiyo yaani kuzaliwa na homoni za kike, ingawa wao ni wanaume kwa muonekano wa nje.

“Kuna hali ya kupambana ambayo nao wanaendelea nayo ndani hasa wale ambao wamezaliwa na homoni za jinsia tofauti na tunavyowaona, wengine wanasema kwa watu wao wa karibu kama wazazi wao na wengine wanapelekwa hata hospitali,” anasema Kimangale.

Anasema wale ambao ushoga unatokana na kujifunza na sababu nyingine za kimazingira ikiwemo udadisi, mara nyingi hujificha na hawapendi kujulikana, hivyo hufanya vitendo hivyo kwa siri.

“Kuna watu wengine wanaoanza tabia hiyo kutokana na mazingira kama kubakwa au kulawitiwa na mwishowe wanazoea mchezo huo, kisaikolojia inaelezwa kuwa ni rahisi kuendelea na ushoga,” anasema.

Daktari wa Magonjwa ya Ndani kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Elisha Osati anasema kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika zikiwemo za hapa nchini, idadi kubwa ya wanaojihusisha na ushoga wana maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama ukimwi na homa ya ini aina B na C ikilinganishwa na watu wengine.

Dk Osati ambaye pia ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), anasema katika njia ya haja kubwa, mara nyingi wanaofanya vitendo hivyo hupata tatizo la kulegea misuli na kushindwa kubana haja kubwa.

Anasema: “Wakati mwingine, huchanika njia ya haja kubwa, kupata uvimbe au mrija wa haja kubwa kutoka nje.”

“Kwenye njia ya haja kubwa ya mtu ilivyoumbwa ina mpira ambao unabana sana na haitarajii kupata usumbufu mkubwa, ikipata mara kwa mara kama ambavyo wanafanya tendo lile mashoga njia hiyo badala ya kukaza, inalegea na wakati mwingine wanashindwa kubana hata ‘choo.”

Osati anasema hata wanawake wanaofanya ngono kinyume na maumbile hupata uvimbe, kuchanika au mrija wa haja kubwa nje na kushindwa kurudi ndani hali ambayo pia huwapata mashoga wengi.

Anasema mambo yanayohusishwa na mtu kujihusisha na ushoga kuwa ni pamoja na mambo ya kibaiolojia vikiwamo vinasaba, homoni yaani vichocheo vya mwili na pia mazingira.

Kibaolojia mtu kabla hajazaliwa vinasaba vyake vinaweza kuhusianishwa, “wataalamu wamefanya tafiti mbalimbali wakiangalia vinasaba wakaangalia chromosomes (chembechembe zinazotengeneza vinasaba) zilizopo ndani ya vinasaba ambavyo kama ikitokea tatizo inaweza kusababisha kupata hali ya kupenda kuwa shoga.”

Anasema imebainika kuwa, takriban asilimia 70 ya watu wenye tabia ya ushoga kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, wana matatizo ya chromosomes.

Aidha Dk Osati anasema katika homoni, ikitokea mwanaume akiwa na homoni za kike (estrogen) kwa wingi maana yake itamfanya awe na matendo ya kike na hivyo kuweza kujihusisha na ushoga.

Kuhusu mazingira, Dk Osati anasema tafiti nyingine zimeonesha kuwa, ni moja ya sababu zinazoweza kumfanya mwanaume kuwa shoga.

Anatoa mfano wa mtoto aliyelelewa katika mazingira ya ushoga au kuchezewa maumbile yake kwamba, ni rahisi kukua na kuendeleza ushoga.

Via Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post