MWENYEKITI IRAMBA ASHAURI BIASHARA YA UKAHABA IHALALISHWE


Mwenyekiti wa halmashauri ya Iramba mkoani Singida, Simon Tyosela ameishauri Serikali kuhalalisha biashara ya akina dada wanaoujiuza, maarufu kama "madada poa" au makahaba.
 
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua ukusanyaji mapato ya halmashauri mbalimbali nchini.


Alitoa ushauri huo juzi kufuatia kauli ya Mkuu wa mkoa, Dk Rehema Nchimbi kueleza kuwa “madada poa”  na “machangu doa”  wote mjini watakamatwa. Dk Nchimbi alitoa kauli hiyo wakati wa Kikao  Maalum cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichoitishwa kupitia na kupitisha Mpango wa bajeti kwa Mwaka 2019/2020

Tyosela alisema kuwa kutokana na halmashauri nyingi nchini kukwama kukusanya mapato, ingekuwa jambo jema kama Serikali ingehalalisha biashara ya "madada poa"  kama zilivyo  biashara nyingine.
  
"Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niseme sikubaliani kamwe na suala la ushoga. Lakini hili la madada poa nashauri lirasimishwe ili Serikali iweze kujipatia mapato" alisema Tyosela na kuongeza,

Iwapo watashindwa kulipa kodi hiyo, basi watakuwa wamejiondoa kwa hiara yao wenyewe kwenye biashara
hiyo badala ya utaratibu uliopo wa polisi kuwakamata.

Hata hivyo, Meya wa Manispaa ya Singida, Gwae Mbua alipinga vikali ushauri huo kwa madai kuwa hatua hiyo itadhalilisha Taifa letu.

"Wanaojiuza ni ndugu zetu, dada zetu na watoto wetu..... Kwa kweli wamekuwa wakitutia aibu. Sikubaliani na wazo la Mwenyekiti wa Iramba kuhalalisha biashara hiyo kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wa Mtanzania" alisema na kuongeza;


Naomba Wabunge waliopo humu wajifanye kama vile hawajasikia ushauri wa ndugu yangu huyu. Kuna namna nyingi za halmashauri kujipatia mapato, kinachotakiwa ni watendaji wetu kuwa wabunifu zaidi katika kubuni vyanzo vipya halali vya mapato na sio hii ya kuuza miili".


Awali, akifungua Kikao hicho Maalum cha RCC, Mkuu wa Mkoa Dk Nchimbi alisema kuwa hakuna Taifa linaloweza kuwa nchi ya viwanda na kuingia kwenye uchumi wa kati kwa kuendekeza vitendo vya kipuuzi kama vile akina dada kujiuza miili yao.


Alisema katika kuhakikisha mkoa unakuwa tulivu na unashughulika zaidi na maendeleo ya wananchi, umejipanga ipasavyo kuwaondosha akina "dada poa" wote mitaani na kwamba tayari wafanyabishara hiyo haramu 38 waliweza kukamatwa kwa siku moja tu.  
 Na Abby Nkungu, Singida

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527