WADAU WAPENDEKEZA SHERIA YA NDOA IFANYIWE MAREKEBISHO

Shirika lisilo la kiserikali la Agape mkoani hapo ambalo linajishughulisha na kutetea haki za watoto, limeilalamikia Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo wameitaja kuwa kikwazo katika mapambano ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga. 

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za mwaka 2012, Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa tatizo la ndoa za utotoni kwa asilimia 59, ikifuatiwa na Mara (55) na Dodoma (51), huku asilimia za kitaifa zikiwa ni 37.

Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa miradi kutoka Shirika la Agape, Mustapha Isabuda, kwenye semina na waandishi wa habari mkoani Shinyanga kuhusu kushirikiana kwa pamoja kupaza sauti kwa kutumia kalamu zao, kuipinga sheria hiyo ambayo imekuwa chanzo cha ndoa za utotoni.

"Katika kutekeleza miradi yetu ya kupinga mimba na ndoa za utotoni mkoani hapo tangu tulipoanza kufanya kazi mwaka 2009, kikwazo kikubwa ambacho kimekuwa kikitukwamisha kutokomeza tatizo hili ni Sheria ya Ndoa Namba 5 ya mwaka 1971 hasa kipengele cha 13 na 17, ambayo ina ruhusu mtoto kuolewa kwa ridhaa ya wazazi au mahakama," alisema Isabuda.

"Tunaomba waandishi wa habari kwa kuwa nyie ni muhimili wa nne wa nchi ambao siyo rasmi, tushirikiane kwa pamoja kupaza sauti kwa serikali ili sheria hii ipate kufanyiwa marekebisho na hatimaye kumaliza tatizo hili la ndoa za utotoni, ambalo limekuwa likizima ndoto za wanafunzi," aliongeza.

Pia alisema sheria hiyo inaweza kukwamisha mpango kazi wa serikali kitaifa (MTAKUWWA), kufikia malengo yake ya miaka mitano ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ambao umelenga kupunguza takwimu za ndoa za utotoni kutoka asilimia 37 hadi kufikia 10, mwaka 2022.

Kwa upande wake wakili wa kujitegemea mkoani Shinyanga, Maria Mwaselela, kutoka ofisi ya Mwaselela (Advocate), akiwasilisha mada alisema sheria hiyo inapaswa kufanyiwa marekebisho ya haraka kutokana na changamoto ya kuendesha kesi za ndoa za utotoni.

Na Marco Maduhu - Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post