MATUMAINI YA KUPATA TIBA YA UKIMWI YAZIDI KUONGEZEKA


Juhudi za kusaka tiba ya ugonjwa wa Ukimwi zinaendelea miongoni mwa wanasayansi ulimwenguni, huku taarifa za matumaini kuhusu upatikanaji wake zikizidi kujitokeza.


Tanzania haijaachwa nyuma katika jitihada za kukabiliana na Ukimwi baada ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kutoa taarifa hivi karibuni kuhusu hatua walizofikia katika kusaka chanjo dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, wanasayansi kutoka Muhas wamekuwa wakitafiti chanjo ya VVU, wakihusisha maofisa wa polisi katika utafiti wao.

“Matokeo ya awali ya utafiti huo yanaashiria kwamba Tanzania inaweza kufikia hatua ya kuvumbua chanjo dhidi ya VVU ikiwa tafiti za ziada zitafanyika,” alisema Profesa Eligius Lyamuya, mratibu wa utafiti huo, wakati akiwasilisha mada yenye kichwa kisemacho “Tulipotoka, Tulipo na Tunapoelekea”.

Huku wataalamu nchini wakiendelea kusaka chanjo, habari za matumaini kutoka jijini London, Uingereza zilisema juzi kuwa mgonjwa aliyekuwa akiishi na VVU ameonekana kupona Ukimwi baada ya kupandikizwa uboho (bone marrow) kutoka kwa mtu mwingine.

Kiongozi wa jopo la madaktari waliomtibu mgonjwa huyo, Profesa Ravindra Gupta, ambaye ni mtaalamu wa baiolojia ya VVU, ameeleza kuwa mgonjwa aliyepewa huduma ya kupandikizwa uboho, ameondolewa virusi lakini akaonya kuwa ni mapema kusema amepona kabisa.

“Hakuna Virusi vya Ukimwi ndani yake ambavyo tunaweza kuvipima na kubaini. Hatuwezi kuona chochote… lakini ni mapema kusema kuwa amepona kabisa,” alisema Profesa Gupta kama alivyokaririwa na AFP.

Jumanne ijayo, wataalamu waliomtibu mgonjwa huyo wanatarajiwa kutoa undani wa taarifa hizo katika jarida la kisayansi la Nature na pia kuwasilisha mada kuhusu ‘uponaji’ katika mkutano utakaojadili virusi aina ya retrovirues na maradhi nyemelezi, utakaofanyika Seattle, Marekani.

“Hii inaonyesha kwamba tiba si ndoto,” alisema mmoja kati ya wanayansi hao, Dk Annemarie Wensing wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Uholanzi.

Hii ni kwa mara ya pili dunia inajulishwa uwezekano wa mgonjwa mwenye VVU kuonekana amepona. Mgonjwa wa sasa ambaye ni wa London, Uingereza na wa Berlin, Ujerumani aliyekuwa anatibiwa saratani 2007 wote walipandikizwa uboho ili kutibu saratani na si VVU.

Na Syriacus Buguzi, Mwananchi 
Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post