TCRA YATOA UFAFANUZI KUHUSU KUPUNGUZA GHARAMA ZA KUSAJILI MITANDAO YA KIJAMII 'BLOGS & ONLINE TV"

Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema  haiwezi kuzungumzia chochote kuhusu gharama za usajili wa mitandao ya kijamii inayotoa maudhui mtandaoni kwa sababu ni sheria na ili kupunguza gharama hizo lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa kupitia bungeni.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya utangazaji kupitia Televisheni na Redio za kawaida na mitandaoni (Blogs & Online Tv) kutoka Kanda ya Ziwa Victoria uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Mhandisi Mihayo alitoa kauli hiyo akijibu swali la Mmiliki wa Malunde Media (Malunde 1 blog), Kadama Malunde aliyeiomba TCRA kupunguza gharama za usajili wa Mitandao ya Kijamii ili kuwasaidia vijana walioamua kujiajiri kupitia mitandao waendelee kutoa huduma za maudhui mtandaoni.

"Hizi gharama wanazotozwa hawa watoa huduma za maudhui mtandaoni ni ndogo ukilinganisha na zile gharama zinazolipwa na watu wa Televisheni na Radio, kwanza watu wa Mtandaoni wana leseni ya kimataifa, anapochukua habari anaenda kuzipakia kwenye mtandao zinaonekana dunia nzima lakini nyinyi (Tv na Radio) mna leseni kulingana na eneo husika",alisema Mhandisi Mihayo.

"Kwa hiyo Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA)  hatuwezi kuzizungumzia chochote hizi gharama za usajili kwa sababu ni sheria,sisi tunatekeleza sheria,kwa hiyo hizi gharama nafikiri ukitaka zipungue ni lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa sababu lazima upitie bungeni",alieleza Mihayo.

Awali akitoa taarifa ya vituo vya utangazaji wa maudhui Kanda ya Ziwa, Mhandisi Mihayo alisema mpaka sasa TCRA inasimamia vituo 36 vya Redio, Televisheni 3 na watoa huduma wanne wa maudhui mtandaoni waliosajiliwa kwa mujibu wa sheria ambao ni Mohab Online Tv, Geita Online Tv, Binagi Blog na Malunde Media.

"TCRA inaendelea na zoezi la kuwabaini watoa huduma mtandaoni ambapo mpaka sasa Kanda ya Ziwa tulishawatambua 24 na kuwatahadharisha kuacha kuvunja sheria kati yao wapo waliotii agizo la Mamlaka kwa kusitisha kwa muda upakiaji wa habari mtandaoni na wanaendelea na taratibu za usajili",alisema.

"Wengine wameendelea kukaidi agizo la mamlaka na kuendelea kuvunja sheria kwa kisingizio eti wanaandika habari za viongozi mbalimbali wa mikoa na wilaya,niwakumbushe viongozi hao kuwa sheria ya usajili wa watoa huduma mtandaoni za Online Tv, Blogs,Online radio,simulcasting online Tv na Radio,Weblogs ipo kwa ajili ya wote zikiwemo taasisi za serikali.

Hivyo basi TCRA inawashauri viongozi waache kusaidia kuvunja sheria ama kwa kujua au kwa kutojua kwa kuwatumia waandishi wanaopakia habari za matukio mbalimbali yanayowahusu kwenye mitandao ya kijamii inayotakiwa kusajiliwa,tutaendelea kuwachukua hatua za kisheria ili kila mtoa huduma mtandaoni anafanya kazi kwa kufuata sheria"

"TCRA inawafahamu watu wote wanaopakia maudhui mtandaoni hivyo wale wanaoendelea kutoa maudhui mtandaoni ni lazima wafuate taratibu za kisheria ikiwemo kujisajili,tunaendelea kuwafuatilia na watashughulikiwa na vyombo vya kisheria",aliongeza.

"Kuna wale ambao wameamua kuhamishia kazi  za blogs Instagram na  Facebook, hawa nao tutawashughulikia",alisema Mhandisi Mihayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527