TCRA YAZIFUNGIA SIMU MILIONI 1.6 ZA WIZI

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezifungia simu 1,682,667 zilizokuwa zikitumika kwenye mitandao mbalimbali ambazo zilibainika kutokuwa na sifa zikiwamo kutofikia viwango vinavyotakiwa, zilizoibwa na zilizoripotiwa kupotea.

Takwimu hizo zitolewa jana na Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba wakati akiwasilisha taarifa juu utendaji kazi wa Mfumo wa Kuratibu na Kusimamia Mawasiliano ya Simu(TTMS) kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) waliotembelea ofisi za mamlaka hiyo.

Alisema kasoro za simu hizo zimebainika kupitia mtambo wa TTMS ambao pamoja na mambo mengine ina moduli ya CEIR(Central Equipment Identifications Register) ambayo ina kipengele cha kutambua taarifa za laini za simu(sim card profile) na namba tambulishi za mawasiliano.

“Moduli ya CEIR imewezesha kuzifungia simu 1,682,667 zilizokuwa zikitumika kwenye mitandao mbalimbali, idadi hii inajumuisha simu zilizobainika kutofikia viwango vinavyotakiwa, simu zilizonakiliwa namba tambulishi(IMEI) pamoja na zile zilizoropitiwa kuibwa ama kupotea,” alisema Kilaba.

Alisema mtambo huo pia umewezesha kubaini mawasiliano ya simu za kimataifa zinazoingia kwa ulaghai ambako mpaka sasa yamepungua na kufikia chini ya asilimia 10 kwa mwaka jana kutoka asilimia 65 mwaka 2013.

Alisema mfumo huo umeonyesha miamala ya fedha iliyofanywa na kampuni za simu ambayo imefikia Sh bilioni 8.9 kutoka Novemba 2014 hadi Februari 2019 ilyozalisha faida ya Sh trilioni 2.5.

Kilaba alisema mfumo huo pia unatoa takwimu za huduma za mawasiliano ya simu za sauti, matumizi ya data na ujumbe mfupi pamoja na fedha zinazopatikana katika kila kampuni ya simu kupitia miamala ya fedha na upigaji wa simu.

Na Aziza Masoud - Mtanzania 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post