RAIS WA TFF WALLACE KARIA AWASHUKURU WATANZANIA KUIUNGA MKONO TAIFA STARS

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) ametoa shukrani za dhati kwa Serikali,Taasisi Mbalimbali,Vyombo vya Habari,Vyombo vya Usalama na kila Mtanzania kwa kuiunga mkono Timu ya Taifa “Taifa Stars”.

Amesema TFF inaamini kila mmoja alihamasika kuiunga mkono Taifa Stars hasa kutokana na kiu ya kila mmoja kuona inacheza AFCON.

“Hakika ilikuwa hamasa kubwa na Uzalendo wa hali ya juu ambao unapaswa kupongezwa kwa namna ambavyo kila mmoja alijitoa kwa nafasi yake kwaajili ya timu yake ya Taifa” Amesema Rais wa TFF Ndugu Karia.

Uungwaji mkono uliofanyika kwa Taifa Stars ni sehemu kubwa ya morali kwa wachezaji na TFF inaamini Watanzania wataendelea kuziunga mkono timu za Taifa na Wawakilishi wa Tanzania wanaokabiliwa na mashindano ya Kimataifa.

Kwasasa timu ya Taifa ya Wanawake “Twiga Stars” ipo Kambini ikijiandaa na mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu Olympic dhidi ya DR Congo utakaochezwa April 5,2019,Pia timu ya Vijana U17 “Serengeti Boys” ipo Kambini ikijiandaa na mashindano ya AFCON ya Vijana U17 yatakayofanyika Tanzania April 14-28,2019.

Karia amewaomba Watanzania waziunge mkono timu hizo kwa kujitokeza kwa wingi ili kuwa sehemu ya hamasa ya kufanya vizuri kwa timu zetu.

TFF itaendelea kuhakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ili kupata matokeo chanya katika mashindano yanayowakabili.

Ni Imani ya TFF kuwa Watanzania wataendelea kujitokeza kwa wingi Uwanjani kuziunga mkono timu zetu kama ilivyokua kwa Taifa Stars.

Vyombo vya Habari ambao ni moja ya Wadau wakubwa tunaamini tutaendelea kushirikiana katika kuhamasisha pia kwa timu zilizopo Kambini

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post