ZITTO KABWE AELEZEA MAANA YA 'SHUSHA TANGA PANDISHA TANGA'


Kumekuwapo na misemo mingi katika siasa ambayo imekuwa ikitumiwa na wanasiasa katika vipindi fulani.

Miongoni mwa misemo ni ule ambao Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliwahi kusema kwamba endapo atafanikiwa kuingia pale magogoni katika jumba jeupe, basi yeye itakuwa ‘Kazi na bata’.

Msemo huo ulipokewa kwa hisia tofauti. Wapo waliopongeza na wengine kusema utawezekanaje iwe kazi na bata. Hilo likapita.

Sasa umeingia mwingine. Huu wa sasa ambao umekuja baada ya vigogo waliokuwa Chama cha Wananchi (CUF) akiwamo aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kutimkia ACT-Wazalendo umekuwa ukitumiwa wa ‘pandisha tanga shusha tanga’.

Unaweza kujiuliza, huu msemo una maana gani, kwa nini ‘shusha tanga na pandisha tanga?

Mwananchi limezungumza na Zitto kuhusu huo msemo amesema, “Kwenye jamii za bahari au ziwa maboti huwa na Tanga.”

“Tanga ni kitambaa kikubwa cha kusukuma majahazi kwa upepo. Tanga likiharibika unalishusha unapandisha tanga jipya.”

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini anasema, “Shusha tanga (shusha CUF) pandisha tanga (pandisha ACT-Wazalendo). Safari iendelee.”

Katika mizania hiyo ya ‘shusha tanga na pandisha tanga’, kesho ngome ya vijana Taifa ya ACT Wazalendo itawapokea waliokuwa viongozi wa kitaifa wa baraza la vijana CUF (JUVICUF).

Shughuli hiyo itafanyika makao makuu ya chama hicho Kijitonyama jijini Dar es Salaam kuanzia saa 5:00 asubuhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post