KAMPENI YA SBL YA ‘UNYWAJI KIISTARABU’ YATUA MAKAO MAKUU YA SERIKALI DODOMA


Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) ACP Nuru Selemani akitoa maelekezo kwa dereva bodaboda Noel Mazengo wakati wa ugawaji wa vifaa vya usalama barabarani (Reflectors) zilizotolewa na Kampuni ya bia ya Seregeti kupitia kampeni yake ijulikanayo kama ‘Usinywe na Kuendesha Chombo cha Moto’ iliyozinduliwa jana Ijumaa Mkoani humo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) ACP Nuru Selemani akipeana mkono na dereva bodaboda Noel Mazengo baada ya kumkabidhi koti la usalama barabarani (Reflector) ikiwa ni Kampeni ya kampuni ya bia ya Serengeti (SBL)iitwayo‘Usinywe na Kuendesha’ inayolenga kupunguza ajali zitokanazo na ulevi hapa nchini.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) ACP Nuru Selemani (Kushoto), Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) John Wanyancha (katikati) na mmoja wa Maofisa wa usalama barabarani wakizungumza jambo mara baada ya kuzindua kampeni ya unywaji kiistarabu iitwayo ‘Usinywe na Kuendesha’ mkoani humo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Dodoma ACP Nuru Selemani na Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) John Wanyancha wakiwa na baadhi ya maderava bodaboda mkoani Dodoma baada ya kuwakabidhi makoti ya usalama barabarani ikiwa ni sehemu ya kampeni ijulikanayo kama ‘Usinywe na Kuendesha’ inayoratibiwa na Kampuni hiyo.
Washiriki wa mkutano wa wadau wa usafirishaji wakisikiliza elimu juu ya unywaji kiistarabu kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya bia ya Serengeti wakati wa uzinduzi wa kampeni ijulikanayo ‘Usinywe na Kuendesha’ mkoani Dodoma.
****
Dodoma, Machi 22, 2019: Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeendesha kampeni yake ya unywaji kiistarabu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani hapa Mkoani Dodoma, makao mapya ya Serikali huku madereva wakinufaika na vifaa vya usalama barabarani.

Kampeni hiyo maarufu kama ‘Usinywe na Kuendesha Chombo cha Moto’ imelenga kuwafikia watu 1,000 wakiwamo madereva hususan bodaboda, wanafunzi wa vyuo pamoja na umma kwa lengo la kutoa elimu juu ya unywaji kiistarabu ili kupunguza ajali zitokanazo na ulevi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika leo katika Hoteli ya Morena jijini hapa, Mkurugenzi wa Uhusiano wa SBL, John Wanyancha alisema kampeni hiyo imelenga katika utoaji elimu kwa wateja wake nchini ili kupunguza matukio yanayoepukika kama ajali zitokanazo na unywaji wa pombe kupindukia.

“SBL imejidhatiti katika kuunga mkono juhudi za Serikali, watu binafsi, wadau na makampuni kuhakikisha kwamba jamii hasa madereva ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo waathirika wa ajali zitokanazo na ulevi, wanazingatia unywaji kiistarabu kwa usalama wao na abiria,” alisema Wanyancha.

Kampeni hiyo inashirikisha wadau mbalimbali ikiwamo Jeshi la Polisi-Kikosi cha usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), madereva bodaboda pamoja na jamii kwa ujumla ikilenga katika kupunguza ajali zitokanazo na ulevi wa kupindukia nchini.

Kwa upande wake,Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) ACP Nuru Selemani amesema kampeni hiyo ni chachu katika kupunguza ajali huku akiwataka madereva kuzingatia elimu iliyotolewa ili kuongeza usalama wao wawapo barabarani.

“Kulishirikisha jeshi la polisi, kikosi cha usalama barabarani, kunaonyesha ni kwa jinsi gani SBL wanatilia maanani suala zima la usalama barabarani hasa matokeo ya ulevi na uendeshaji vyombo vya moto. Uzoefu unaonyesha kwamba baadhi ya watu hujisahau na kujiingiza katika ulevi wa kupindukia bila kuzingatia usalama wao na wa vyombo vya moto wanavyoendesha”, alisema

Kwa mujibu wa ripoti za Jeshi la Polisi-Kikosi cha Usalama barabarani kwa mwaka 2018, jumla ya ajali 876 za bodaboda ziliripotiwa kutokea na kusababisha vifo 366 na majeruhi 694. Ripoti zinaonyesha kupungua kwa ajali hizo ambapo kwa mwaka 2017 zilikuwa 1,459 zilizosababisha vifo 728.

Ili kupambana na ajali hizo, SBL imekabidhi jumla ya makoti ya usalama barabarani (Reflectors) 80 kwa madereva bodaboda ili kuhimiza uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani.

RTO aliwataka madereva kutumia makoti hayo ipasavyo kila wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku kwa usalama wao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.

MWISHO


Kuhusu SBL:

Ikiwa imeanzishwa kama Associated Breweries mwaka 1988, Kampuni ya Bia Serengeti (SBL) ni moja ya kampuni kubwa za bia nchini Tanzania, ambapo aina zake za bia zinachangia zaidi ya asilimia 20 ya bidhaa hizo katika soko.

SBL inaendesha viwanda vitatu vilivyopo Dar es Salaam, Mwanza na Moshi.

Tangu kuanzishwa kwa SBL mwaka 2002 biashara yake imekua na kuimarika zaidi na asilimia 51 ya hisa mwaka 2010 zilizochukuliwa na Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL) zimeshuhudia ongezeko la uwekezaji katika kukua zaidi na hivyo kusababisha kuongezeka kwa fursa zaidi za ajira kwa watu wa Tanzania. 

Aina za bia zinazozalishwa na SBL ambazo zimepata tuzo kadhaa za kimataifa ni pamoja na Serengeti Premium Lager, Pilsner, Tusker Lager, Tusker Lite, Kibo Gold, Guinness stout, Uhuru na Kick.

SBL pia ni wazalishaji vinywaji vikali vinavyofahamika duniani kama vile Johnnie Walker Whisky, Smirnoff Vodka, Gordon’s Gin, Captain Morgan Rum na Baileys Irish Cream.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527