TUNDU LISSU AFUNGUKA 'YA NASSARI KUNG'OLEWA UBUNGE"


Nimesoma yanayomhusu Joshua Samwel Nassari, mbunge wa Arumeru Mashariki, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuhusu kuvuliwa ubunge wake. Nimeona hapa kuna mwelekeo mkubwa wa kukubaliana na hukumu ya Spika Job Ndugai, kwamba Mheshimiwa Nassari hajahudhuria Mikutano Mitatu Mfululizo ya Bunge, kwa hiyo amepata anachostahili.

Baadhi wameenda mbali zaidi na kudai Nassari ‘amevuta mpunga’ na kuuza jimbo. Wengine wamesema, “ni maandalizi ya ‘kuunga mkono juhudi,’ na mengineyo. 

Katika yote haya, sijasikia yeyote akidai kujua upande wa Nassari mwenyewe una msimamo gani. Tumekimbilia kwenye hukumu kutokana na maneno ya Spika na tafsiri zetu wenyewe. Hii sio sawa sawa.

Binafsi, nimewasiliana na Josh Nassari jana usiku. Amenitafuta mwenyewe kunitaka ushauri. Kwa maneno yake mwenyewe, hii habari ya kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge sio ya kweli.

Ameniambia alihudhuria vikao vya Bunge la Novemba mwaka jana, na alisaini na kulipwa posho zake kama kawaida. ‘Vikao vya Mkutano’ ni pamoja na vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, kwa mujibu wa tafsiri ya neno ‘kikao’ katika Kanuni za Kudumu za Bunge.

Kama anayoyasema Mh. Nassari ni ya kweli, basi kuna ziada kubwa ya maneno tusiyoijua katika jambo hili. Sio sahihi kurukia kwenye hitimisho bila kusikiliza upande wake.

Pili ni kuhusu barua yake ya tarehe 29 Januari mwaka huu. Mh. Nassari ameniambia alikuwa anamuuguza mke wake ambaye alipata matatizo makubwa ya uzazi wakati anajifungua tarehe 27 Januari.

Siku iliyofuata, tarehe 28 (siku ya kuanza vikao vya Bunge) aliwasiliana na msaidizi wa Spika Ndugai. Akashauriwa na msaidizi huyo (Said Yakob) kumwandikia Spika Ndugai juu ya suala lake, na akafanya hivyo kesho tarehe 29 Januari.

Majibu ya barua ya Mh. Nassari kwa Spika Ndugai, ni taarifa yake ya jana ya kumfuta Ubunge.

Sasa hapa kuna suala la tafsiri ya sheria. Je, kama ni kweli Spika Ndugai aliandikiwa barua ya kuombwa ruhusa katika mazingira hayo ya dharura na hakuijibu? Je, hicho kimya chake kina maana gani kisheria? Is it not the case of ‘silence means consent’ here?

Jambo la tatu ni la utaratibu wa uamuzi wenyewe. Spika Ndugai hajamuandikia au kuwasiliana kwa namna yoyote ile na Mh. Nassari ili kumjulisha juu ya hatua anazotaka kumchukulia kwa kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge.

Ni kweli kwamba Ibara ya 71 ya Katiba ya Jamhuri, haijaweka utaratibu wa Spika kumwandikia au kumjulisha Mbunge juu ya hatua anazopanga kumchukulia kwa kutohudhuria mikutano ya Bunge.

Je, ukimya huo wa Katiba una maana Spika Ndugai hawajibiki na hakuwajibika kumjulisha Mh. Nassari kabla ya kumfuta Ubunge?

Hili ni suala lingine la tafsiri ya sheria. ‘Natural justice’, misingi ya haki ya asili, inamtaka mtoa maamuzi yeyote yanayoweza kuathiri haki ya mtu mwingine, kumpa mtu huyo fursa ya kujitetea kabla ya uamuzi utakaomwathiri kutolewa.

Masharti haya ya haki ya asili ni ya lazima hata pale ambapo sheria haijaweka utaratibu huo. ‘Audi alteram partem’, ‘sikiliza upande mwingine.’ Huo ndio msimamo wa kisheria wa Tanzania hii.

La mwisho ni huu utaratibu wa Spika Ndugai kuwasiliana na mitandao ya kijamii au hadharani badala ya kuwasiliana kwanza na Mbunge anayehusika kwanza.

Mheshimiwa Nassari ameniambia amesikia taarifa za kufutwa Ubunge wake mitandaoni kama wewe na mimi. Na mimi nilisikia habari ya kufutiwa mshahara na posho za kibunge mitandaoni.

Je, huu ni utaratibu sahihi wa Spika wa Bunge kuwasiliana na Wabunge kuhusu masuala yao ya kibunge? Yote haya ni masuala muhimu kuyaangalia kabla ya kukimbilia kwenye hukumu kwamba Mh. Nassari ‘ameuza Jimbo’, au amekosea, n.k.

Tutayajua mengi sana endapo Mh. Nassari atafungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kufutiwa Ubunge, kama ambavyo nimemshauri. Tuvute subira.
Mwandishi wa makala hii, Tundu Lissu, ni mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, mwanasheria mkuu wa Chadema na wakili wa Mahakama Kuu. Kwa sasa, yuko kwenye matibabu nchini Ubelgiji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post