WAZIRI MKUU : MSIBA WA KIBONDE UMETUSHTUA SANA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kifo cha aliyekuwa Mtangazaji Muandamizi wa kituo cha redio cha Clouds, Ephraim Kibonde ni pengo kubwa kwa Taifa, Clouds Media Group na tasnia ya habari kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 8, 2019) alipokwenda kuhani msiba wa Mtangazaji Muandamizi kituo cha redio Clouds, Kibonde kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Mbezi Beach Dar es Salaam.Kibonde alifariki dunia jana alfajiri Machi 7, 2019 jijini Mwanza.

“Msiba huu umetushtua sana na ni tukio ambalo hatukulitarajia ila ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Hivi karibuni sote tulimshuhudia akiongoza ratiba ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba na alienda hadi Kagera kumzika.”

Waziri Mkuu amesema marehemuKibonde enzi za uhai wake ameshirikiana vizuri na Serikali katika shughuli mbalimbali, hivyo amewaomba wananchi waendelee kushikamana na kuifariji familia. “Tumuombee marehemu apumzike kwa amani.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wazazi, watoto wa marehemu pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa na subira na watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao. 


(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527