ASKARI POLISI AKUTWA AMEKUFA BAA

Askari Polisi, PC Donald Motoulaya (29) wa ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, amekutwa amefariki dunia akiwa kwenye baa iitwayo Friends Pub iliyopo Manispaa ya Songea mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma, ACP Simon Marwa alisema tukio hilo limetokea Machi 13,2019 saa 4:30 usiku.

Kamanda Marwa alisema Motoulaya kabla ya kufariki dunia, alianguka kwenye ngazi za mlango wa baa hiyo baada ya kujikwaa.

Kamanda huyo alisema mhudumu aliyejulikana kwa jina la Jaibu Nyoni (26), alimtoa nje na alifika kwenye Baa hiyo akitokea Baa ya karibu aliyoitaja kwa jina la Yapenda au Mtini pub kwa lengo kujipatia kinywaji zaidi.

“Baada ya kutolewa nje huku mhudumu akiendelea na shughuli zake, askari huyo alijipenyeza na kuingia kwenye chumba cha ndani cha baa hiyo na kwenda kukaa eneo lililowekwa makochi. Huyu askari alikuwa ameyazoea mazingira ya baa hiyo, hivyo alikaa huko bila wahudumu kufahamu kama yupo,” alisema kamanda huyo.

Walibaini kuwa kuna mtu ndani kwenye kochi na amelala asubuhi walipokuwa wanafanya usafi.

Kamanda Marwa alisema wahudumu hao waliingiwa na hofu baada ya kumuita lakini hakuitika wala kuamka, ndipo wakaamua kutoa taarifa kituo kuu cha polisi cha mjini Songea.

Na polisi walipofika wakabaini kuwa askari huyo alikuwa amefariki dunia na kuuchukua mwili wake kwenda kuuhifadhi Hospotali ya Songea (Homso).

Na  Joyce Joliga, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post