TRAFIKI WALIOWASHUSHIA KIPIGO, MATUSI DEREVA NA ABIRIA WAKAMATWA


Jeshi la Polisi nchini, linawashikilia askari wake wawili wa Kitengo cha Usalama Barabarani kwa makosa ya kushambulia kwa matusi na kipigo dereva wa gari na abiria wake.

Tukio hilo lilianza kusambaa juzi kupitia video fupi iliyokuwa ikitumwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha askari hao wawili wakimtukana dereva na kumpiga yeye na abiria wake wakati walipokuwa wakishuka kwenye gari mara baada ya kusimamishwa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamadi Masauni, alitoa agizo la kukamatwa kwa askari hao kutokana na askari hao kukosa uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa mafunzo na uchoraji picha za usalama barabarani yanayotolewa na Kampuni ya Mafuta ya Puma kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, tukio hilo halikubaliki na ndio sababu wamewachukulia hatua za kisheria.

Masauni alisema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi ya madereva kubambikiwa makosa au askari kufanya vitendo vilivyo kinyume na mwenendo mwema wa jeshi hilo na hivyo walipoona tukio hilo waliwachukulia hatua askari hao ambao wapo kituoni kusubiri taratibu za kisheria.

Alisema vitendo hivyo vinajumuisha upokeaji wa rushwa, lugha chafu kwa madereva pamoja na kuwashambulia ni kinyume cha sheria.

“Jana kuna video ambayo ilikuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha askari wakimtukana dereva pamoja na abiria waliokuwamo na si hivyo tu ilifika hatua hadi kumpiga. Baada ya tukio hili nilimuagiza Kamanda wa Kiko cha Usalama Barabarani achukue hatua kwa suala hili. Na jana (juzi) nilipewa taarifa wamekamatwa askari waliofanya kitendo kile na wamewekwa ndani na sasa wanasubiri kufikishwa kwenye vyombo vya sheria," Masauni alisema.

Alisema hao wapo kituo cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wakisubiri kuchululiwa hatua na kuwataka wananchi wote pindi wanapoona kuna vitendo ambavyo wanafanyiwa vilivyo kinyume cha sheria zetu wasisite kutoa taarifa kwetu.

Alisisitiza kuwa ikitokea uongozi wa askari unatetea au kutochukua hatua muafaka, mlalamikaji apande uongozi wa juu hata kwa Waziri na Naibu wake ili hatua zichukuliwe.

“Ninawaasa askari wote kuwa serikali iko makini na haitaruhusu mwananchi yoyote aonewe na vyombo vya dola hali kadhalika hatutaruhusu mwananchi au taasisi yoyote imuonee askari kwa sababu yoyote ile,” alisema Masauni.

Akizungumzia suala la usalama barabarani, Masauni aliishukuru Kampuni ya Mafuta ya Puma, kwa kuendesha program hiyo na alizitaka kampuni zingine kuiga mfano huo kwa kuwekeza kwenye ulinzi na usalama wa watoto ambao ni taifa leo na kesho.

Alisema Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama Barabarani wana program nyingi za kusaidia kutoa mafunzo kwa shule zote zilipo kwenye mazingira hatarishi na zisizo kwenye mazingira hayo pia.

“Programu hizo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali za kifedha. Ninaomba kutumia fursa hii kuomba uongozi wa Puma kukisaidia Kikosi cha Usalama Barabarani kuzifikia shule zote nchini kwa kupitia askati walioko kwenye maeneo yote nchini," Masauni alisema.

Pia alimuagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuanza mchakato wa kuandaa andiko la kutoa mafunzo kwa shule zote nchini na kuliwasilisha Puma ili wasaidie kuokoa ajali za barabarani kwa wanafunzi kwa njia ua mafunzo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Puma, Dominic Dhanah, alisema kuwa mafunzo hayo yanakwenda sambamba pia kwa wanafunzi waliowahi kufundishwa.

Alisema madhumuni ya kuwahusisha wanafunzi wa shule za msingi, wanaamini kuwa watoto hao wanakabiliwa na hatari za ajali za barabarani na kuhitaji mafunzo ya usalama barabarani ili kuepuka ajali.

“Usalama barabarani ni kipaumbele namba moja katika Kampuni ya Mafuta Puma na tumeamua kuwafundisha watoto wadogo kwani tunfahamu hatari za barabarani wanazokabiliana nazo.

“Tumefanya utafiti na kugundua kuwa shule tulizoendesha mafunzo haya , ajali kwa wanafunzi zimepungua na hivyo basi kwa mwaka 2019 mafunzo haya yataendeshwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar,” alisema Dhanah.

Chanzo- NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post