WAHUNI WAIBA MAGURUDUMU YOTE YA GARI NA KULITUNDIKA JUU YA MAWE

Jamaa mmoja eneo la  Donholm jijini Nairobi nchini Kenya sasa anapanga kuhama baada ya wahuni kuiba magurudumu yote ya gari lake usiku na kulitundika juu ya mawe.

 Inadaiwa kuwa, jamaa huyo ambaye jina lake halikutajwa aliamka asubuhi na kuvaa suti yake tayari kwenda kazini lakini alipofika eneo la maegesho yake mtaani Donholm, alipigwa butwaa kwani magurudumu ya gari lake hayakuwapo na gari hilo lilikuwa liking’inia juu ya mawe. 

 Wizi wa vifaa vya magari yaliyoegeshwa mitaani unasemekana kuvuma sana maeneo ya Donholm, Kayole, Githurai, Dandora na mitaa mingineyo jijini Nairobi.

 Kisa hicho kilichowashtua hata majirani zake walioteremka kutoka katika nyumba zao kuja kushuhudia, kiliwaacha na mshangao mkubwa. 
Kulingana na walioshuhudia, hii sio mara ya kwanza kwa tukio la aiana hiyo kutokea mtaani humo na mitaa ya karibu na kwamba juhudi za kuwakamata wahuni hao hazijafua dafu. 

 “Hawa jamaa wamekuwa wakifanya hivi kwa muda, wanaiba kisha wanazama lakini katika siku za karibuni wamekuwa wakiiba siku baada ya siku.

 Hata juzi waliiba mtaa jirani,” alisema mmoja wa wakazi mtaani humo ambaye hakutaka jina lake kutajwa kwa kuhofia usalama wake. 

Katika picha iliyochapishwa Facebook na Sarah Ndungu, Jumatatu, Februari 18 gari linaloaminiwa kuwa la jamaa huyo ambalo linaonekana likiwa juu ya mawe ishara kwamba magurudumu yake yalikuwa yameng’olewa.

 Baadhi ya waliochangia jumbe kuhusu kisa hicho walionyesha hali ya kushangaa na pia kuna aliyewahi kukumbwa na hali kama hiyo. 

 Picha inayoonyesha jinsi wezi huwaibia wenye magari usiku na wanapoamka asubuhi hukutana na picha ya kutisha.

 Katika hali ya kuzuia wizi zaidi, wengi wa wakazi mtaani humo sasa wanaweka vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ving’ora, kamsa na kamera za cctv kukabiliana na wezi hao.

 Inadaiwa zamani wezi walikuwa wakiiba sana magurudumu ya ‘spare’ na betri lakini siku hizi huhakikisha wanaondoka na kila kitu na kuliacha gari lao juu ya mawe .

Vifaa vinavyoibwa kutoka kwenye magari huuzwa kwa bei ya kutupa katika baadhi ya maduka ya kuuza vipuri vya magari. 

Inaelezwa kwamba utashi mkubwa wa vifaa vya magari umechangiwa mno na idadi kubwa ya magari yanayoingizwa nchini, na hivyo kuwafanya wahuni kuwa na soko tayari la vifaa vya wizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527