AJALI YA COASTER NA LORI YAUA ABIRIA WOTE KWENYE COASTER


Watu 19 wakiwemo wanaume 15 na wanawake wanne wamefariki dunia papo hapo baada ya basi aina ya Toyota Coaster mali ya Kampuni ya Komkia lililokuwa likisafiri kutokea Jijini Mbeya kwenda Tunduma, mkoani Songwe kugongwa kisha kulaliwa na lori lililokuwa likitokea Tunduma kwenda Dar es salaam.

Ajali hiyo ilitokea jana katika eneo la mlima Senjele uliopo wilayani Mbozi kilometa chache kutoka mpakani mwa Mbeya na Songwe, ambapo inadaiwa lori hilo lilishindwa kusimama na kuligonga lori jingine lililokuwa limebeba shehena ya mahindi likitokea mkoani Songwe na kuligonga basi hilo na kisha kulilalia basi hilo lililokuwa na abiria 17 ambao wamekufa wote.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Hery Kagya amethibitisha kupokea miili 17 ambayo imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa wa Songwe na miili mingine miwili imehifadhiwa katika hospitali ya Ifisi katika mji mdogo wa Mbalizi.

“Miili ya abiria hao ambao imekatikakatika vipande vipande isipokuwa watu wawili ambao ni mwanamke na mwanaume ambaye ni dereva wa lori aliyekuwa na mwanamke huyo, wote hawajatambulika walikimbizwa katika Hospitali ya IFISI Jijini Mbeya walikufa muda mfupi wakati wakipatiwa matibabu na kufikisha vifo 19,” amesema Dk Kagya.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Yusuf Abdi alisema lori hilo ambalo lilikuwa nyuma ya lori lingine lililobeba shehena ya mahindi, kabla ya kugongana na basi lililigonga lori lililobeba mahindi na kisha kugongana na Coaster na kulilalia.

“Sikuweza kujua chanzo cha ajali mara moja, lakini ninachoweza kusema ni madereva waongeze umakini wanapoendesha magari na kuacha kuendesha kwa mazoea,” alisema Abdi.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali mstaafu, Nicodemus Mwangela ambaye alikuwa mmoja wa watu waliofika kuokoa majeruhi katika ajali hiyo alisema alipokea taarifa ya ajali hiyo muda wa saa nne usiku na kufika eneo la tukio mara moja.

Alisema ajali hiyo ni moja ya tukio baya kutokea mkoani humu tangu Januari mwaka huu.

Aidha amewapongeza wananchi na askari wa Jeshi la Polisi waliofika usiku huo ili kuokoa majeruhi na kuweka hali ya utulivu ili kuruhusu njia kupitika na watumiaji wengine.

Na  Stephano Simbeye, Mwananchi









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post