MFANYABIASHARA ATEKWA AKINUNUA JENEZA ARUSHA

Mfanyabiashara wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Jeremiah Simon(49) mkazi wa Sekei wilayani Arumeru, anadaiwa kutekwa wakati akiwa katika eneo la mochwari, Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa maandalizi ya kununua jeneza.


Simon ni Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini (brokers) mkoani Arusha.

Imeelezwa kuwa mfanyabiashara huyo alitekwa kutoka katika eneo hilo Jumatatu, Januari 28, mwaka huu, majira ya jioni.

Kwa mujibu wa mke wake , Janet Jeremia, mumewe alichukuliwa na watu wasiofahamika akiwa na mtu mwingine aitwaye Loth Greyson ambaye ni jirani yake. Imeelezwa kuwa watekaji hao waliokuwa kwenye gari aina ya Land Cruiser nyeupe, baada ya siku moja walimwachia Loth kwa sharti la kutozungumza chochote juu ya tukio hilo.

Janet alisema tangu siku hiyo hadi sasa hajui mume wake alipo ila siku ya Jumanne, Januari 29 mwaka huu, alimpigia simu na kumweleza kuwa yupo salama na baada ya hapo hakuweza kumpata tena kupitia mawasiliano hayo.

Awali, shuhuda wa tukio hilo ambaye ni fundi wa kutengeneza majeneza eneo hilo, Salimu Mzirai alisema siku hiyo lilikuja gari aina ya Landcruiser rangi nyeupe na waliteremka watu wapatao watatu na kuwachukua watu wawili akiwemo mfanyabiashara huyo.

Kaimu Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani hapa, Longinus Tibushubwamu, alithibitisha tukio hilo na kueleza wapo katika hatua ya uchunguzi.

Kwa upande wake, kaka wa mfanyabiashara huyo aitwaye Joseph Simon, mkazi Simanjiro Manyara alisema alipata taarifa za kutoweka kwa mdogo wake siku ya Jumatatu jambo ambalo limewaumiza.

Hata hivyo, Loth alipopatikana hakuweza kuzungumzia tukio hilo japo alithibitisha kutekwa na watu wasiojulikana na hakutambua walipelekwa wapi kwa kuwa alikuwa amefungwa kitambaa usoni.

Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527