Treni ya kwanza ya mwendokasi nchini India imeanguka jana Jumamosi baada ya kugonga ng'ombe aliyekuwa kwenye reli, ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Mkuu Narendra Modi kuzindua huduma ya abiria.
Treni hiyo, Vande Bharat Express, ambayo inachukuliwa kuwa ni treni ya mwendo kasi kuliko zote nchini India na iliyojengwa chini ya kaulimbiu ya Serikali ya Modi ya "Make in India (Tengeneza Ndani ya india)", ilifanya safari yake ya kwanza Ijumaa ikitoka New Delhi kwenda Varanasi, ambao ni mji mtakatifu wa Hindu.
Lakini wakatio ikirejea kwenye mji huo mkuu wa India siku iliyofuata, iligonga ng'ombe na hivyo ajali hiyo kutibua ugavi wa umeme katika mabehewa manne na hivyo kuharibu breki, kwa mujibu wa Shirika la Reli la India.
"Baadaye treni ilipata matatizo ya kiufundi na hivyo kusimama wakati ikiwa njiani kwenda Delhi," msemaji wa shirika hilo, Smita Sharma aliiambia AFP.
Treni hiyo ilifika Delhi salama, ikiwa ni kabla ya kuanza safari za kibiashara leo, aliongeza.
Mifugo imekuwa tatizo kubwa katika barabara za India na kwenye reli nchini India, hasa katika jimbo la Uttar Pradesh ambako ajali hiyo imetokea leo.
Tangu aingie ofisini, chama cha Modi kimeanzisha mkakati wa kuzuia kuchinja ng'ombe ambao wananchi wengi wa India huchukulia kuwa ni kitu kitakatifu-- jambo lililosababisha idadi ya mifugo hiyo kuongezeka.
Kwa sasa India inafanya jitihada kubwa za kuboresha usafiri wa reli uliojengwa enzi za ukoloni na ambao miundombinu yake imechoka, kwa ajili ya kusaidia usafiri wa watu milioni 23 kwa siku.
Treni hiyo iliyotengenezwa India ina kasi ya kilomita 180 kwa saa, ikiwa ni kasi ya asilimia 20 zaidi ya treni nyiungine ya kasi inayofanyiwa matengenezo.
Mamlaka zinasema treni hiyo inatarajiwa kupunguza safari ya kilomita 850 baina ya miji hiyo mikubwa miwili kutoka saa 14 hadi nane.