AFISA WA POLISI AMWAGA MACHOZI MTOTO WA MIAKA 6 AKIAPISHWA KUWA POLISI


Askari Polisi wa Marekani ametokwa machozi wakati akimwapisha kwa heshima mtoto Abigail Arias (6) kuwa polisi.


Mtoto huyo anayesumbuliwa na saratani ya kibofu kwa miaka miwili sasa alihudhuria hafla hiyo ya kuapishwa akiwa na familia yake, huku akisema anaipenda kazi hiyo na ataifanya kwa weledi.

Polisi wa Texas, walituma taarifa za kumwapisha mtoto huyo katika hafla iliyofanyika mjini Texas kuwa polisi wa mji wa Freeport wenye watu 12,000 uliopo maili 50 kutoka Kusini mwa Houston.

Polisi amwaga machozi

Ofisa wa polisi aliyekuwa akimwapisha mtoto huyo alishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa kwikwi huku akimkumbatia baada ya kumaliza kumwapisha.

“Nitapambana na wahalifu’’ hayo ni maneno ya mtoto huyo aliyotoa baada ya kuapishwa huku akishangaza wengi waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo

Wakati akiapishwa mtoto huyo alikuwa amevalia vazi la polisi ambalo lilimpendeza na kumfanya kuwa na faraja wakati wote wa hafla hiyo iliyokuwa imehudhuriwa na familia yake pia na maofisa kadhaa wa polisi.

Mama mzazi wa mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Ilene Arias, aliliambia Shirika la Habari la CNN kwamba huu ni muda wa kufurahia maisha ya mtoto huyo kwani watalia wiki chache zijazo.

Mama huyo alitoa kauli hiyo huku akiwa anabubujikwa na machozi mbele ya waandishi wa habari, akimaanisha kwamba mtoto wake huyo hawezi kuendelea kuishi kwa muda mrefu.

Kilio cha mama huyo kinakwenda sawa na polisi aliyekuwa akimwapisha ambaye alishindwa kujizuia na kuanza kulia Kamanda huyo wa Freeport, Raymond Garivey, alisema mtoto huyo anaishi kwa nguvu za Mungu tu.

“Tunatakiwa kumuombea mtoto huyu kwa sababu inafahamika anaumwa kitu gani hapa anaishi kwa miujiza tu, hivyo tumuombee,’’ alisema.

“Nataka kuhakikisha ndoto zake zinatimia na kuwa za kweli hivyo leo tumemwapisha kuwa askari kamili wa Marekani kwa sababu ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu,’’ alisema.

Baada ya kuapishwa kuwa askari Arias alikabidhiwa ofisi na bunduki kama walivyo askari wengine huku akionyesha tabasamu.

Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post