ALIYEONDOLEWA JELA KWA MSAMAHA WA RAIS AKAMATWA NA SARE ZA JWTZ

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia aliyekuwa mfungwa katika Gereza la Segerea na kuachiwa kwa msamaha wa Rais mwaka jana, Emmanuel Magoti (18), kwa tuhuma za kukutwa na sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini humo, Kamishna wa Polisi, Lazaro Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Januari 30, mwaka huu, saa 8 mchana eneo la Mbagala. Alisema Polisi ilimkamata kijana huyo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kwamba amekuwa akijihusisha na makosa ya uhalifu ndani ya kanda hiyo huku akiwa amevaa sare za JWTZ.

“Lengo la mtuhumiwa huyu ni kujificha baada ya kutenda makosa hayo ili lawama ziwaendee wanajeshi hao. Tulivyopata taarifa hizo tulianza ufuatiliaji mara moja na kwa bahati tulimkamata na tulimkuta akiwa na sare hizo ambazo ni suruali mbili, koti moja na fulana,” alisema. Alieleza kuwa makachero wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari polisi wa JWTZ (MP) walifika katika nyumba ya mtuhumiwa huyo na kukuta sare hizo.

Alifafanua kuwa katika mahojiano na mtuhumiwa huyo alikiri kujihusisha na matukio ya uhalifu akishirikiana na wenzake wawili ambao walifanikiwa kutoroka na kwamba wanaendelea kuwafuatilia. “Mtuhumiwa huyu alikiri kwamba alikuwa mfungwa katika gereza la Segerea kwa kosa la wizi na kwamba aliachiwa kwa msamaha wa Rais mwaka 2018.

Msako mkali unaendelea kuwatafuta wenzake wawili wanaoshirikiana nao katika matukio hayo,” alieleza. Mambosasa alitoa onyo kwa wafungwa wanaotoka magerezani kwa rufaa, msamaha wa rais au kumaliza vifungo, kuacha kujihusisha na matendo hayo kwa sababu wanakuta hali shwari lakini wanachochea mitandao ya uhalifu.

Alisisitiza kuwa lengo la msamaha ni kumfanya mtu aliyejutia arudi kwa jamii kuungana nao kufanya shughuli za jamii na kwamba wanachotegemea ni mabadiliko ya tabia wanapofanya mafunzo jela ili aweze kupata maarifa waweze kuishi kama raia wema wanaofuata sheria. Kwa mujibu wa Mambosasa, wafungwa wanaotoka gerezani na kuanzisha makundi ya uhalifu watambue kwamba jeshi hilo liko macho kwani wataendelea kufuatilia ili kuwalinda raia wema dhidi ya wahalifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527