WENYE MAKALIO MAKUBWA WAFUNGUKA KUNYANYASWA MITAANI

 Umekuwa ni utani wa kawaida kukohoa, kupiga kelele au kufanya vituko vingine kila wanawake wenye makalio makubwa wanapopita sehemu yenye watu wengi, lakini sasa wamechoshwa; hawataki kero hiyo.

Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe amesema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wanawake na watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo, ikiwa ni pamoja na kushikwa miili yao na kuzomewa kutokana na maumbile yao.

Profesa Mwamfupe alisema hayo jana alipokuwa akifungua warsha ya siku moja kuhusu utekelezaji wa mradi wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto wenye umri chini ya miaka 15 hadi 49 unaofanywa katika maeneo ya wazi.

Mradi huo unaendeshwa na Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa (UN Women) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (Alat).

Alisema kuna ongezeko kubwa la vitendo visivyofaa katika jamii kama ulevi uliopindukia, utumiaji wa dawa za kulevya, ukabaji, uporaji na uvaaji wa mavazi yasiyozingatia maadili.

“Wanawake wengine wanadhalilishwa kutokana na maumbile yao, jambo ambalo ni kikwazo kwa uhuru wao,” alisema.

“Ni wakati kwa jamii nzima kupaza sauti kupambana na hali hii yenye athari kwa maendeleo ya wanawake.”

Alisema kero hiyo pia inathibitishwa na utafiti wa Tanzania Demographic Survey wa mwaka 2015/2016 unaoonyesha kuwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 umefikia asilimia 40.

Baadhi ya wanawake wenye makalio makubwa waliohojiwa na Mwananchi baada ya ufunguzi wa hafla hiyo, walionyesha kukerwa na vitendo hivyo.

Walisema vitendo hivyo vimekithiri katika baadhi ya maeneo hususani katika vituo vya daladala, hali inayosababisha wakose amani. “Tabia hii hasa ipo kwa vijana na watu wengine wakubwa ambao naona hawajiheshimu,” alisema Janet Caren, mkazi wa Dodoma.

Huku akionyesha kukerwa na vitendo hivyo, Caren alisema watu hao hutoa maneno ya ovyo dhidi ya wanawake wa aina hiyo.

“Hatukuomba kuwa na maumbile haya,” alisema msichana huyo, akishauri Serikali iangalie jinsi ya kukomesha tabia hiyo.

Mwanamke mwingine, Joyce Matewa pia mkazi wa jijini hapa, alisema kuna siku alikuwa akipita barabarani akasikia sauti ikitokea ndani ya daladala ikisema “dada umeangusha”, lakini hakuwa amebeba mzigo wowote.

Na Nazael Mkiramweni, Mwananchi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post