WAKAZI WA TINDE KUPATA HUDUMA YA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) amewahakikishia wakazi wa Tinde halmashauri ya Shinyanga kuwa maji kutoka Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria utaanza kutekelezwa hivi karibuni baada ya wataalamu Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kahama Shinyanga (KASHWASA) kupita kila kitongoji katika kata ya Tinde kubaini maeneo ambayo yatawekwa maghati ya kuchotea maji.

Azza ameyasema hay oleo Februari 21,2019 wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi kijiji cha Nyambui na Jomu vilivyopo katika kata ya Tinde halmashauri ya Shinyanga.

Akijibu swali kutoka kwa wananchi waliohoji ni lini wakazi wa Tinde watatuliwa kero ya maji ambayo kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaika nayo, Mhe. Azza alisema serikali imesikia kilio chao na sasa tayari wataalamu kutoka KASHWASA wamepita Tinde kubaini maeneo ambako yatawekwa maghati na ndipo mwananchi ambaye atahitaji kuvuta maji kupeleka nyumbani kwake atavuta kutoka kwenye maghati hayo.

“Naridhishwa na jinsi serikali inavyoendelea na utekelezaji wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwani mwanzoTinde ilionekana kusahaulika…

“Mara kadhaa nimekuwa nikilisemea bungeni na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipopita Tinde Mwezi Julai nilimkumbusha suala la maji kwenye mkutano wa hadhara kwani hapa Tinde tuna changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama na ukiangalia Tinde ni Mji unaokua kwa kasi”,aliongeza.

Awali,kabla ya Mbunge huyo kuanza kujibu maswali juu ya kero ya maji, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uswahilini Hemed Rashid alisimama na kueleza kuwa tayari wataalamu kutoka KASHWASA wameshapita kwenye kitongoji chake kubaini maeneo ambapo wataweka maghati ya maji.

Naye Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huo kwa kutozuia maeneo yao kupitishwa mabomba.

“Toeni ushirikiano, huenda kuna watu wakazuia mabomba yasipite kwenye maeneo yao,hii haitapendeza… ukizuia maana yake unazuia watu wengine wasipate maji, niwaombe sana tutoe ushirikiano,mradi huu ni mkubwa na maji yatapita Tinde,tutakuwa na maji safi na salama”,aliongeza Mboneko.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi Tinde. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko,kulia ni Mwenyekiti wa kijiji cha Jomu,George Masele- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Azza Hilal Hamad (CCM) akizungumza na wakazi wa Tinde.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza katika mkutano wa hadhara Tinde
Wakazi wa Tinde wakiwa kwenye mkutano.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uswahilini Hemed Rashid akielleza kuwa tayari wataalamu kutoka KASHWASA wameshapita kwenye kitongoji chake kubaini maeneo ambapo wataweka maghati ya maji.
Wakazi wa Tinde wakiwa kwenye mkutano wa hadhara.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527