MKURUGENZI WA MABASI YA MWENDO KASI KORTINI KWA KUSABABISHA HASARA YA BILIONI 2

Mkurugenzi wa UDART, Robert Kisena(46) na wenzake watatu wamesomewa mashitaka 19 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiwemo utakatishaji fedha wa Mil.603 na kuisababishia hasara UDART ya Bil.2.41.


Mbali ya Kisena, Washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Cheni Shi (32).

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali, George Barasa, Ester Martin, Moza Kasubi na Imani Imtumezizi.

Barasa alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka hayo likiwamo moja la kuongoza uhalifu, kujenga kituo cha mafuta bila kibali, kuuza mafuta sehemu zisizoruhusiwa, wizi wakiwa wakurugenzi, mashtaka manne ya utakatishaji fedha, manne ya kughushi, manne ya kutoa nyaraka za uongo, mawili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na moja la kuisababishia mamlaka hasara.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 kwa mamlaka waliyokuwa nayo waliusababishia mradi wa UDART hasara ya Sh.bilioni 2.41.

Katika shtaka lingine, ilidaiwa kuwa mshtakiwa wa kwanza na wanne, Robert na Shi, wanadaiwa kati ya Mei 26, 2016, wakiwa benki ya NMB tawi la Ilala, wakiwa wakurugenzi wa Kampuni Longway Engineering huku Kisena akiwa Mkurugenzi wa UDART walifanya muamala wa Sh. milioni 603 kupitia akaunti ya benki ya UDART kisha kuzihamishia fedha hizo katika akaunti ya Longway na baada ya siku mbili wakijua fedha ni za kughushi.

Katika shtaka lingine, ilidaiwa kuwa Mei 30, 2016, Robert na Shi katika benki ya NMB tawi la Ilala, walijipatia nyaraka kwa njia ya udanganyifu kutoka katika benki hiyo ikiwa na jina la Fund Transfer Request Form ikiwa na tarehe ya Aprili 6, 2016, kwa lengo la kuonyesha Sh. milioni 750 zimelipwa na Kampuni ya Longway kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa kituo cha UDART Kimara, Kivukoni, Ubungo na Morocco, huku wakijua ni uongo.

Martin alidai shtaka la Robert na Shi, Juni 8, 2016, katika benki ya NMB tawi la Ilala walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh. milioni 595.92 kutoka UDART kwa kuonyesha zimelipwa na kampuni ya Longway ambayo imehusika katika kutengeneza vitu mbalimbali vya mradi huo, huku wakijua ni uongo.

Ilidaiwa kuwa Aprili 6, 2016 katika benki ya NMB tawi ya Ilala, Robert, alighushi nyaraka hiyo kwa lengo la kuonyesha Sh. milioni 594 zimelipwa kwa kampuni ya Longway ambayo imejihusisha na uandaaji, utengenezaji wa vitu mbalimbali wakati ni uongo.

Katika shtaka la kutakatishaji fedha linalowakibili washtakiwa wote wanne, wanadaiwa kuwa kati ya Mei 25, 2015 na Desemba 31, 2016 wakiwa jijini Dar es Salaam kwa nia ovu walibadilisha thamani ya mafuta ya zaidi ya Sh. bilioni 1.21 kuwa fedha ya thamani hiyo baada ya kuyauza mafuta hayo, huku wakijua mafuta hayo ni zao la kosa la wizi.

Kosa lingine ni la kujenga kituo cha mafuta bila kuwa na vibali vya EWURA ambalo linamkabili Robert na Kulwa ambao wanadaiwa walilitenda Januari 1, 2015 na Desemba 31, 2017 maeneo ya Jangwani Ilala.

Inadaiwa kuwa washtakiwa Robert na Kulwa wakiwa wakurugenzi wa Kampuni ya Zenon Oil na Gas Ltd kwa pamoja walijenga kituo hicho cha mafuta bila kuwa na kibali cha EWURA.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na kibali cha kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na uliomba tarehe ya kutajwa.

Hakimu Simba alisema kesi hiyo itatajwa Februari 23, mwaka huu na washtakiwa walipelekwa rumande kwa sababu mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527