ZAHERA : LIVERPOOL WANA NAFASI YA KUICHAPA MAN CITY LEO


Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera

Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera ametoa mtazamo wake kuelekea mchezo mkali wa EPL leo kati ya vigogo Manchester City na Liverpool.

Akizungumza katika mahojiano na Kipenga Extra ya East Afrika Radio inayoruka Jumatatu mpaka Ijumaa, kuanzia saa 6:00 mpaka saa 7:00 mchana, Zahera amesema kuwa anaamini Liverpool wana nafasi ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

"Mechi ya Man City na Liverpool leo, mimi mtazamo wangu naona kwamba City anaweza kupigwa leo, kutokana na mbio za wachezaji wa Liverpool na ile 'Counter Attack' yao, lakini mpira ni kitu cha ajabu, naweza kusema hivi lakini kesho tukakuta kimetokea kingine," amesema Mwinyi Zahera.

"Man City imefungwa mechi mbili hapa karibuni kabla ya kushinda dhidi ya Southampton, Liverpool yenyewe ikishinda michezo mitatu ya nyuma ukiwemo ushindi dhidi ya Arsenal. Naogopa sana kwamba City anaweza kuteseka na mbinu za Jurgen Klopp," ameongeza Zahera.

Liverpool inakwenda katika mchezo huo ikiwa haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa katika EPL, wadau wengi wa soka wakiipa nafasi kubwa kuibuka na ushindi kutokana na rekodi za hivi karibuni za timu hizo kuibeba Liverpool.

Katika mechi 11 za mwisho baina ya timu hizo katika mshindano yote, Manchester City imefungwa mechi 7 na kutoa sare mechi 3 huku ikishinda mara moja pekee ambayo ni msimu uliopita ilipoifunga Liverpool mabao 5-0.

Mechi hii inaweza kutoa picha halisi kwa Liverpool katika kuwania ubingwa, kwani endapo itaibuka na ushindi itamuacha Man City kwa tofauti ya pointi 10, lakini pia Man City endapo itaibuka na ushindi, itaibua matumaini zaidi ya kuikamata Liverpool, kwani itapunguza pengo la alama na kufikia 4.

Chanzo - Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527