Wizara ya Maliasili na Utalii, imeanza kuyatambua na kuainisha maeneo kwa ajili ya utalii wa Fukwe katika Kisiwa cha Mafia mkoani Kibaha kwa ajili ya kuhamasisha Wawekezaji kuchangamkia fursa ya ujenzi wa Hoteli za kitalii ili kuwavutia watalii kutembelea katika kisiwa hicho.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa aliyoyatoa mwaka jana kwa Wizara hiyo kuwa ianzishe Kurugenzi ya Fukwe itakayokuwa na jukumu la kusimamia na kuendeleza Fukwe zote nchini.
Lengo likiwa ni kuhakikisha mapato yatokanayo na sekta ya Utalii kupitia Utalii wa Fukwe yanaongezeka kwa mfano Kisiwa cha Mafia ni cha tano duniani kwa uzuri wa vivutio vya utalii na rasilimali bahari na cha pili barani Afrika, Hivyo kina sifa kemkem za kuongeza pato la Taifa zaidi.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya siku mbili kisiwani humo ya kutembelea Fukwe pamoja na magofu ya kale, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amesema Wizara imejipanga kikamilifu kwa ajili kuwasaidia Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye Fukwe kwa ajili ya utalii.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Kanyasu alitembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii vilivyopo kisiwani humo ukiwemo Msitu wa Mlola, Magofu na fukwe katika kijiji cha Kanga pamoja na maeneo ya uwekezaji ya Ras Mlundo Jojo, Banja, Rasini Kanga na Tembo Unyama.
Hata hivyo, Baada ya ziara hiyo Naibu Waziri huyo alisema kuwa baadhi ya wamiliki wa maeneo hayo ya fukwe yamefanya kuwa mashamba ilhali ni kivutio kikubwa cha utalii ambapo baadhi ya nchi zimekuwa ziikingiza fedha nyingi za kigeni kupitia utalii wa fukwe.
Aidha, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi wanaomiliki maeneo karibu na Fukwe kuyatumia kwa ajili ya utalii wa fukwe badala ya kuyageuza kuwa mashamba.
Amesema kuwa watalii walio wengi kutoka nje za nchi mara baada ya kutembelea Hifadhi za Taifa kama vile Serengeti Mikumi, husafiri kwenda Msumbiji au Zanziba’ kwa ajili ya kutembelea Fukwe ilhali kuna fukwe nzuri mbali na Kisiwa cha Mafia ambazo hazijaweza kuendelezwa
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaib Nnunduma alieleza kuwa wilaya yake inawakaribisha Wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika wilaya hiyo na kuahidi kuwa atatoa ushirikiano wa kutosha.
Aliongeza kuwa Wilaya hiyo tayari imeshatenga maeneo kwa ajili ya Wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli za kiutalii katika maeneo ya ufukweni.