CCM YAWAONYA WALIOTEULIWA NA RAIS MAGUFULI KUANZA KUTAFUTA UBUNGE KABLA YA WAKATI


Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi katika Mji mdogo wa Lamadi, mara baada ya kuwasili Mkoani Simiyu kwa ajili ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoaniSimiyu Januari 05, 2019

Na Stella Kalinga, Simiyu

Katibu Mkuu wa Chama cha Mpinduzi (CCM) Taifa Dkt. Bashiru Ally amewaonya baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, na Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, ambao wameanza kukaa vikao kwa ajili ya kutafuta majimbo kabla ya wakati wa Chama hicho kutangaza mchakato wa kutafuta wagombea wapya wa ubunge na udiwani.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo Januari 05, 2019 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM pamoja na Viongozi na watendaji wa Serikali katika wilaya ya Bariadi na Itilima wakati akiwa katika ziara yake mkoani Simiyu.

Dk Bashiru amesema ikiwa viongozi hao wataendelea kufanya hivyo atawataja hadharani na akasisitiza kuwa ni vema wakaridhika na nafasi walizopewa na Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwani kushindwa kufanya hivyo ni kumdharau aliyewateua.

“Wapo wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, Makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri, na wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wameanza kukaa vikao kwa ajili ya kutafuta majimbo, CCM hatujatangaza mchakato wa kutafuta wabunge au madiwani wapya, uko wakati nitawatangaza hadharani, mridhike na nafasi zenu mlizopewa na Mhe. Rais”, alisema

Katika hatua nyingine Dkt. Bashiru amesema kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu 2019 Viongozi wa CCM wajipange katika kuhakikisha viongozi wa Vijiji na Mitaa wanachaguliwa katika misingi ya demokrasia kwa kuzingatia sifa zao na si fedha zao(rushwa).

“ Katika mwaka huu wa kumuenzi Mwalimu Nyerere baada ya miaka 20 tunataka kufanya mchakato wa kusimamia uchaguzi uwe tofauti, wakati wa kuteua tuzingatie sifa na tuwapime viongozi kwa maisha yao na vitendo vyao......”, alisema Dkt. Bashiru.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi ameishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 26 katika kipindi cha miaka mitatu, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe.Njalu Silanga, ameishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya barabara ambapo amebainisha kuwa kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) barabara katika jimbo hilo zimetengenezwa zinapitika na zipo ambazo zinaendelea kufanyiwa matengenezo.

Naye Katibu wa CCM Mkoa, Bw. Donald Magesa akitoa taarifa ya Chama, utekelezaji wa Ilani ya CCM mkoani humo umefanyika vizuri huku akisisitiza kuwa Viongozi wa Chama na Serikali wamejipanga kwa kushirikiana na wananchi kukamilisha maboma yaliyojengwa ili kila mwanafunzi aliyefaulu darasa la saba mwaka 2018 aweze kuanza kidato cha kwanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post