KATIBU MKUU WA CCM ASHAURI WAKUU WA MIKOA KUJIFUNZA SIMIYU


Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Bashiru Ally amewashauri Wakuu wa Mikoa hapa nchini kwenda(kuja) mkoa wa Simiyu kujifunza namna ya kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kati ya Chama na Serikali sambamba na ubunifu na uchapakazi wa viongozi wa mkoa huo.

Dkt. Bashiru ameyasema hayo Januari 05, 2019 wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM pamoja na Viongozi na watendaji wa Serikali, Mjini Bariadi wakati akiwa katika ziara yake mkoani Simiyu.

Dkt. Bashiru amewapongeza Viongozi wa Serikali wakingozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa namna wanavyoshirikiana na viongozi wa Chama kwa namna wanavyosimamia shughuli za maendeleo.

“Niwapongeze kwa namna mnavyosimamia shughuli za maendeleo, nilikuwa hapa mwaka 2005 kama msimamizi wa uchaguzi nilizunguka maeneo mengi mengine yalikuwa hayapitiki, leo nimekuja nikazungushwa maeneo machache tu, nimeona mambo mengi sana ya tofauti kwa hiyo uongozi wa mkoa huu kwa Chama na Serikali umefanya kazi kubwa na bado mna nafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa zaidi”, alisema.

Aidha, amesema ili uchumi uwe imara, wa kisasa na wenye manufaa ni lazima uwe jumuishi na uwalenge watu walio wengi ambao ni wazalishaji wadogo hususani katika katika sekta ya kilimo na viwanda huku akisisitiza umakini zaidi ili uwepo wa viwanda na maendeleo ya kilimo viwanufaishe wengi.

Ameongeza kuwa wakati Mkoa wa Simiyu unapanga mipango mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi ni vema kukawa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, ili kuondoa migogoro kwa watumiaji ambayo inakuwa chanzo cha chuki na watu kuishi kwa wasiwasi.

Katika hatua nyingine Dkt. Bashiru amesema CCM imejipanga kuhakikisha kuwa itasimamia na kuimarisha ushirika ambao utasimamiwa na wataalam wenye taaluma na maadili ili uweze kuwanufaisha wanaushirika na kutatua changamoto zao.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa Viongozi na watendaji wa Serikali Mkoani humo watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM huku akisisitiza kuwa fedha zote zinazoletwa katika mkoa wa Simiyu zitasimamiwa vizuri na zitafanya kazi iliyokusudiwa.

Aidha, Mtaka amesema Mkoa wa Simiyu unafanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF) ili kubaini fursa za kiuchumi zilizopo katika katika kila kijiji kwa Vijiji vyote 470, ambapo utekelezaji wa Falsafa ya Kijiji Kimoja Bidhaa Moja(OVOP) unatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi Februari.

Ameongeza kuwa viwanda vikubwa vitatu vyenye uwezo wa kuajiri takribani wafanyakazi 2000 kikiwepo kiwanda cha chaki na kiwanda cha vifungashio (Maswa) kiwanda cha bidhaa 18 za afya zitokanazo na pamba(Bariadi) vitajengwa mwaka huu 2019 Simiyu.

“Ndugu Katibu Mkuu mwaka jana wakati Mhe. Rais anapokea ndege ya Air Bus alicheza muziki na ukiangalia ilikuwa ni kitu kinachotoka moyoni kuonesha furaha yake, ninaamini mwaka 2019 Mhe. Rais ataucheza muziki huo hapa Simiyu”, alisema Mtaka.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Simiyu amesisitiza viongozi na wanachama kuimarisha uhusiano mzuri, kusaidiana na kupendana katika maisha ya siasa huku akiwasihi viongozi kulinda na kuheshimu dhamana walizopewa kwa kutimiza wajibu wao.

Akitoa salamu kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, Mbunge wa Bariadi,Mhe. Andrew Chenge ametoa wito kwa viongozi na wanachama wa CCM mkoani Simiyu kudumisha upendo, umoja na mshikamano hususani katika kipindi cha kueleka uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post