YANGA YATOBOLEWA SHINYANGA....STAND UNITED HAWANA MASIHARA


Yanga SC imepoteza mechi ya kwanza ya msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa bao 1-0 na wenyeji, Stand United Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Safari ya kucheza bila kufungwa kwa Yanga katika msimu imeishia katika mechi ya 20 na sasa wanabaki na pointi zao 53, ingawa wanaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 12 zaidi ya Azam FC wanaofuatia katika nafasi ya pili, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wana pointi 33 za mechi 14.

Bao lililoizamisha Yanga SC limefungwa na Nahodha wa Stand United, Jacok Massawe dakika ya 88 akimtungua kwa kichwa kipa Klaus Kindoki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kufuatia krosi ya Mwinyi Elias kutoa upande wa kulia. 

Kama lawama kwa bao hilo, basi ni za mabeki wa Yanga, ambao leo wamechezeshwa wengi zaidi ili kuongeza imara wa safu ya ulinzi, lakini wakamruhusu Massawe kuchomoka katikati yao na kuiunganishia nyavuni krosi ya Mwinyi aliyepasiwa na Six Mwakasega.

Yanga SC ilicheza vizuri leo tangu mwanzo, lakini ilikuwa hovyo katika eneo moja, kwenye umaliziaji, kwani pamoja na kufika mara nyingi kwenye eneo la hatari la Stand walishindwa kufunga.

Na mabadiliko yaliyofanywa na mwalimu Mwinyi Zahera leo, akimtoa Haruna Moshi ‘Boban’ na Mrisho Ngassa na kuwaingiza Mkongo mwenzake, Heritier Makambo na Pius Buswita nayo hayakuwana tija pia.

Siku ya kufa nyani, miti yote huteleza, wachezaji wa Yanga walimlalamikia mara mbili refa kuwanyima penalti baada ya wachezaji wa Stand United kuonkana kuunawa mpira kwenye boksi.

Kikosi cha Stand United kilikuwa; Mohammed Makaka, Mhando Washa, Majaliwa Shaaban, Jisendi Maganda, Ahmed Tajuden, Majjid Kimbondile, Datius Peter/Mwinyi Elias dk51, Hafidh Mussa, Six Mwasekaga, William Kimanzi/Maurice Mahela dk77 na Jacob Massawe.

Yanga SC; Klasu Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Mrisho Ngassa/Pius Buswita dk64, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Amissi Tambwe, Haruna Moshi/Heritier Makambo dk46 na Ibrahim Ajibu.

Via Binzubeiry blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527