NYOTA WA SOKA AFRIKA AFARIKI DUNIA


Phil Masinga

Nyota wa soka wa zamani wa Afrika Kusini na klabu ya Leeds United ya England Phil Masinga, amefariki dunia leo akiwa na miaka 49. 

Chama cha soka nchini humo (SAFA), kimethibitisha na kusema ni siku ya masikitiko kwa taifa hilo kutokana na mchango wake katika soka.

Masinga aliichezea Leeds United katika miaka ya 1994 na 1996 kabla ya kutimkia klabu ya St Gallen nchini Switzerland kisha Salernitana na Bari za Italia.

''Rais wa SAFA Danny Jordaan, amesema Masinga alijitolea kwenye soka la taifa hilo nje na ndani ya uwanja na alisaidia kutangaza vipaji vya taifa hilo, hivyo msiba wake ni wa taifa na ni pigo katika tasnia hiyo'', amesema.


Masinga alicheza mechi yake ya kwanza kwenye timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) mwezi Julai 1992 dhidi ya Cameroon.

Mbali na hilo Masinga anakumbukwa na watu wa Afrika Kusini kwa goli lake dhidi ya DR Congo ambalo liliwezesha taifa lake kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 1998 ambayo ilikuwa mara yao ya kwanza.

Masinga pia alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Afrika Kusini kushinda ubingwa wa AFCON mwaka 1996.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post