SERIKALI YAMJIBU LISSU

Mbunge wa Singida mashariki (Chadema) Tundu Lissu.

 Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas amemjibu mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu, akidai kuwa mwakilishi huyo wa wananchi anazungumza uongo kuhusu maendeleo ya Tanzania.

Dk Abbas amesema kwamba licha ya kuulizwa mazuri ya Serikali lakini Lissu alishindwa kujibu na badala yake aliishia kubabaika.

Akihojiwa na kituo cha Utangazaji Uingereza (BBC) jana Januari 16, 2019, Lissu amezungumza masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na maoni yake kuhusu maendeleo ya nchi, utawala wa katiba na mpango wake wa kugombea urais.

"Unakwenda Ulaya unaponda nchi yako eti haifuati Katiba wakati wewe mwenyewe kuanzia ubunge wako, sifa za ubunge wako na taratibu za uchaguzi wa ubunge wako vyote vipo kwenye Katiba na ndio maana ukawa mbunge,” alisema Dk Abbas.

Dk Abbas amedai Lissu hata alipoulizwa mazuri aliyoyaona licha ya changamoto zilizopo, alishindwa kujibu vyema.

"Angalia alivyoshindwa si tu kueleza jema moja la nchi yake baada ya kupewa fursa hiyo, bali kashindwa hata kueleza jema moja alilofanya yeye binafsi jimboni kwake, kaishia kubabaika tu," amedai Dk Abbas.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina dhamira tofauti na ile waliyonayo watu wa aina ya Lissu, hivyo itaendelea kutekeleza wajibu wake katika kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.

"Sisi tunapigania maendeleo na Watanzania wanaona kazi kubwa inayofanyika kote nchini iwe reli, maji, viwanda, umeme na mambo mengine. Hakuna wa kutuzuia katika kuiletea Tanzania maendeleo. Hakuna,” amesisitiza.

Chanzo:Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post